Pambazuko FM Radio

Ifakara yawatahadharisha wanaokaidi suala la usafi

16 March 2026, 6:51 pm

Picha ya Benedict Ngela afisa afya kata ya Ifakara(Picha na Katalina Liombechi)

Licha ya uwepo wa kampeni mbalimbali za kuhamasisha usafi, uongozi wa kata hiyo pia unasimamia utekelezaji wa sheria ndogo walizojiwekea ili kuhakikisha wale wanaokaidi kanuni za usafi wanachukuliwa hatua stahiki.

Na Katalina Liombechi/David Ngogolo

Uongozi wa Kata ya Ifakara umesema hauna uvumilivu kwa watu wanaochafua mazingira au kukaidi kwa makusudi utekelezaji wa masuala ya usafi ndani ya kata hiyo.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha mazingira ya kata hiyo yanabaki kuwa safi na salama kwa afya ya wananchi.

Akizungumza na Pambazuko FM kuhusu juhudi za kudumisha usafi, Afisa Afya wa kata hiyo, Bwana Benedict Ngela, amesema kuwa wameweka mikakati mbalimbali inayolenga kuhakikisha Ifakara inakuwa safi wakati wote. Alieleza kuwa moja ya mikakati hiyo ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi ili kila mmoja atambue wajibu wake katika kulinda na kutunza mazingira.

Aidha, amesema kama Kata wameanzisha kampeni ya usafi inayofanyika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, ambapo wananchi hushiriki kusafisha maeneo yao pamoja na maeneo ya umma.

Kampeni hiyo imekuwa ikiwahamasisha wakazi wa Ifakara kushiriki kikamilifu katika shughuli za usafi na kuimarisha ushirikiano wa kijamii.

Ngela ameongeza kuwa pamoja na kampeni hizo, uongozi pia unasimamia utekelezaji wa sheria ndogo walizojiwekea ili kuhakikisha wale wanaokaidi kanuni za usafi wanachukuliwa hatua stahiki.

Picha ya Benedict Ngela afisa afya kata ya Ifakara(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Afisa afya

Aidha amesema wamekuwa wakihamasisha matumizi ya mapipa ya kuhifadhia taka, ambapo wafanyabiashara wanaweza kuungana kutumia pipa moja kuhifadhi taka kabla ya kukusanywa na kupelekwa dampo.

Sauti ya afisa afya

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Ifakara wamesisitiza kuwa suala la usafi ni jukumu la kila mwananchi huku wakitoa wito kwa wenzao kuona umuhimu wa kutunza mazingira yao na kushiriki kikamilifu katika shughuli za usafi ili kudumisha afya na ustawi wa jamii.

Sauti za wananchi