Pambazuko FM Radio

Mwanafunzi darasa la sita afariki baada ya Kujinyonga Ulanga

18 February 2026, 7:23 pm

Picha hii sio halisi kutoka sehemu ya tukio(Picha kutoka Mtandaoni)

Tukio hilo ni la kwanza kutokea katika kijiji hicho

Na David Ngogolo/Nicolatha Mpaka

Mtoto wa kike anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 15, mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi Moonlight iliyopo kijiji cha madibila, kata ya Lupiro, Wilaya ya Ulanga amefariki dunia kwa madai ya kujinyonga kwa kutumia kamba za viatu.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Golani Kijiji cha Madibila, Bw. Hamis Kambwili, akizungumza na Pambazuko FM kwa njia ya simu tukio hilo lilitokea Februari 16, 2026 majira ya saa mbili kamili usiku.

Aidha, amewasihi wazazi na jamii kwa ujumla kuwa karibu na watoto wao ili kubaini changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi mapema.

Sauti ya Bwana Hamis Kambwili Mwenyekiti

Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho, akiwemo Khadija Mayambua na Fadhili Rashid Hemed, wamesema wameshtushwa na tukio hilo kutokana na umri mdogo wa mtoto huyo.

Wananchi hao pia wamewataka wazazi na walezi kuwa na utamaduni wa kuzungumza na watoto mara kwa mara, kusikiliza matatizo yao na kuwapatia msaada unaostahili.

Sauti za baadhi ya wananchi kijiji cha madibila

Hata hivyo Pambazuko FM inaendelea kufuatilia taarifa hii kwa mamlaka zinazohusika ili kujua chanzo cha tukio hilo.