Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
11 February 2026, 8:12 pm

Kupitia juhudi hizi, GECA na washirika wake wanaendelea kuweka msingi imara wa kizazi kipya cha wanawake wanasayansi watakaobadilisha dunia.
Na Katalina Liombechi
Wakati Dunia ikiadhimisha Siku ya Wasichana na Wanawake katika sayansi leo Februari 11,2026 Chini ya shirika la UNESCO,Shirika la Girls Education for Climate Action (GECA) Ifakara wamefanya maadhimisho hayo maalum kwa kuwakutanisha wanafunzi wa kike kutoka shule mbalimbali za msingi, sekondari pamoja na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi Shirikishi cha Mtakatifu Fransisko Ifakara (SFUCHAS).
Maadhimisho hayo ambayo GECA wamefanya katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Benignis iliyopo katika halmashauri ya Mji wa Ifakara yamelenga kuhamasisha wasichana na wanawake kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika masuala ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM), sekta ambazo kwa muda mrefu zimeonekana kutawaliwa zaidi na wanaume.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Shirika la GECA, Happyness Ngonyani, amesema lengo kuu la tukio hilo ni kuwahimiza wasichana kujiamini, kuthubutu na kuingia katika sekta ya sayansi bila woga.

Katika tukio hilo, wanafunzi wamepata fursa ya kufanya majaribio mbalimbali ya kisayansi, kujifunza kwa vitendo pamoja na kusikiliza simulizi za wanawake waliofanikiwa katika taaluma za sayansi mafunzo hayo yaliwapa hamasa na kuwajengea imani kuwa ndoto zao zinawezekana.

Wanafunzi wa Chuo cha Udaktari cha SFUCHAS walioshiriki katika maadhimisho hayo akiwemo Grace Yuda,Lovenes Mdidi na Glory Kiyenzi wamesema safari yao haikuwa rahisi, kwani walikumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo kukatishwa tamaa na mitazamo hasi ya kijamii huku wao walichagua kusimama imara na kupigania ndoto zao.

Maadhimisho hayo kwa mwaka huu 2026 inafanyika chini ya kauli mbiu isemayo “Muunganiko wa akili unde,sayansi ya jamii,STEMi na fedha kuelekea dira ya 2050:Kujenga mustakabali jumuishi kwa wanawake na wasichana” yameacha ujumbe mzito kwa jamii kuwa ni wakati wa kuvunja vikwazo vinavyowazuia wasichana kushiriki kikamilifu katika sekta ya sayansi na kutoa fursa sawa kwa wote.