Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
9 February 2026, 8:09 pm

“Tunawakaribisha wawekezaji kuja kulima mazao ya kimkakati katika wilaya ya Kilombero”
Na Katalina Liombechi
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, amewataka wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza katika Wilaya ya Kilombero kutokana na uwepo wa fursa nyingi za kiuchumi pamoja na mazingira rafiki ya uwekezaji.
Wito huo ameutoa leo Februari 9, 2026, wakati akiongoza kikao cha Baraza la Biashara la Wilaya pamoja na Kamati ya Ushauri Wilaya DCC na Bajeti kilichofanyika katika Ukumbi wa Mlimba, uliopo Ifakara.
Amesema Kilombero ina rasilimali za kutosha katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, biashara na viwanda, huku Serikali ikiendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji ili kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Mwenyekiti wa Chama cha wakulima,wafanyabiashara na wenye viwanda TCCIA Wilaya ya Kilombero ameishukuru serikali kwa ushirikiano wanaoupata huku wakiendelea kuiomba kuweka mazingira wezeshi na kutatua changamoto zao kwa wakati ili wajivunie kuwekeza Kilombero.

Akifunga Kikao hicho Mkuu wa Wilaya Kyobya amepongeza uwasilishaji wa bajeti za Tsh.Bil 72 Ifakara na Bil 42 Mlimba huku akieleza kuyachukua mambo yaliyokuwa na maswali mengi na kuahidi kuyapeleka ngazi ya juu Ikiwemo changamoto ya miundombinu ya barabara,malalamiko ya wakulima wa miwa na changamoto ya Tembo.