Pambazuko FM Radio

TESIFA yawapa matumaini mapya vijana 144

19 October 2025, 11:53 pm

Picha na Katalina Liombechi

Mafunzo hayo ambayo yametolewa na taasisi ya TESIFA Tanzania kwa kushirikiana na Swisscontact chini ya shirika la maendeleo nchini Uswiss (SDC) Kupitia ubalozi wa Uswiss Tanzania yamelenga kuwawezesha vijana hao kujipatia ujuzi utakaowasaidia kujitegemea, kujisimamia kimaisha, na pia kuwa mfano wa mafanikio kwa wengine katika jamii

Na; Katalina Liombechi

Katika jitihada za kuwawezesha vijana kujitegemea kiuchumi na kijamii, vijana 144 kutoka kata sita Halmashauri ya mji wa Ifakara wamepata matumaini mapya kupitia mafunzo ya ufundi wa kushona, chini ya mradi wa stadi za maisha uliofadhiliwa na Ubalozi wa Uswiss hapa nchini.

Mkuu wa wilaya wakili Dunstan Kyobya (mwenye shati la mikono mirefu kushoto) Picha na; K. Liombechi

Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo hayo, mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, aliwapongeza vijana hao kwa kujitokeza na kutumia fursa hiyo kwa manufaa ya maisha yao ya sasa na baadaye.

Sauti ya mkuu wa wilaya wakili Danstan Kyobya

Kupitia risala iliyosomwa na Mwajuma Ibrahim Juma na Mariam Mmbaga, Mratibu wa Mradi wa SET kutoka TESIFA Tanzania, ambaye alieleza kuwa mradi huu ni sehemu ya juhudi endelevu za kuwawezesha vijana wa Kitanzania kupata ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na kujiajiri ambapo katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara vijana hao ni kutoka kata za Kibaoni, Mbasa, Lumemo, Lipangalala, Viwanjasitini pamoja na kata ya Ifakara.

Sauti ya Mariam Mmbaga

Baadhi ya wazazi wa vijana hao waliishukuru taasisi ya TESIFA pamoja na wadau wa maendeleo kwa kuleta mradi huo Ifakara, wakisema kuwa hatua hiyo imeleta faraja na matumaini kwa familia nyingi.

Sauti ya wazazi

Nao vijana waliopata mafunzo hayo walieleza kwa furaha kuwa wamejengewa msingi thabiti wa maisha na kushukuru kwa kupatiwa vifaa vya kuanzia, kama sehemu ya mtaji wa kuanza shughuli zao na kupambana na hali ya maisha.

baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo; Picha na Katalina Liombechi
Sauti ya vijana waliohitimu

Mradi huu unaendelea kuwa dira ya mafanikio kwa vijana wengi nchini, huku ukilenga kuwaunganisha na fursa zaidi za kiuchumi na kijamii.