Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
19 September 2025, 10:32 am

Wananchi wa Kijiji cha Sululu wilayani Kilombero wameeleza kero ya tembo kuharibu mazao na mzigo wa kuchangia walimu wa kujitolea. Mkuu wa wilaya, Wakili Dunstan Kyobya ameahidi hatua za haraka kutatua changamoto hizo.
Na: Kuruthum Mkata
Wananchi wa Kijiji cha Sululu, Kata ya Signal katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara, wilayani Kilombero, wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo tembo kuvamia mashamba na kuharibu mazao pamoja na michango ya mara kwa mara kwa ajili ya walimu wa kujitolea shuleni
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara kijijini hapo, baadhi ya wananchi akiwemo Asha Athuman Kiiga na Salum Kibandike wamesema kuwa tembo wameharibu mazao yao yote, na licha ya kutoa taarifa kwa maafisa wa wanyamapori, hawajapata msaada wowote, bali wamekuwa wakizungushwa. Pia wametaja kuwa wanachangia fedha kwa ajili ya walimu wa kujitolea, jambo linalowapa mzigo wa kiuchumi.
Akijibu changamoto hizo, mkuu wa milaya ya Kilombero, wakili Dunstan Kyobya, katika mkutano wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi, amesema serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan si ya uonevu wala ya wizi. Akiwa mkutanoni, alimpigia simu mtaalamu wa Maliasili na kumpa siku moja kuhakikisha malalamiko ya wananchi wa Sululu yanafikishwa wizarani kwa hatua zaidi.

Kuhusu suala la michango kwa walimu wa kujitolea, DC Kyobya alisema si kosa iwapo jamii imekubaliana kuchangia kwa hiari, hasa wakati huu serikali ikiendelea kujipanga kuongeza rasilimali watu katika sekta ya elimu. Alisisitiza kuwa mambo lazima yaendelee huku serikali ikiboresha huduma hatua kwa hatua.