Pambazuko FM Radio

SIDO yawezesha wajasiriamali Ifakara

18 September 2025, 10:53 am

washiriki wa semina wajasiriamali – picha na; Jackline Jerome

SIDO Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali imeendesha semina ya siku tatu kwa wajasiriamali, wawekezaji na wenye viwanda Ifakara, kwa lengo la kuwawezesha kupata ujuzi wa kukuza biashara na kuepuka migogoro ya kikodi na changamoto za usajili wa biashara.

Na: Isidory Mtunda

Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Morogoro limeendesha semina ya siku tatu kwa wajasiriamali, wawekezaji na wenye viwanda katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara, kwa lengo la kuwawezesha kupata maarifa ya kukuza biashara zao na kuondokana na changamoto mbalimbali za kibiashara.

Kaimu mkurugenzi halmashauri ya mji Ifakara; Said Majaliwa Mohamed – Picha na Jackline Jerome

Akifungua semina hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Bw. Saidi Majaliwa Mohamed, amewataka washiriki wa semina hiyo kuzingatia mafunzo hayo kwani yatasaidia kuwaondoa kwenye umasikini. Amesisitiza kuwa umasikini hauondolewi kwa kupewa pesa, bali kwa kupatiwa ujuzi utakaowasaidia kuzalisha. 

sauti ya bw. Saidi Majaliwa Mohamed- kaimu mkurugenzi Ifakara mji

Meneja wa SIDO mkoa wa Morogoro, Bi. Joan Nangawe, akiwasilisha mada katika semina hiyo, amesema shirika lao linahudumia wajasiriamali wa ngazi mbalimbali—kuanzia wenye mitaji midogo hadi wakubwa waliothubutu kuanzisha viwanda, ambao wote ni wanufaika wa huduma zao. 

Meneja wa SIDO mkoa wa Morogoro; Joan Nangawe – Picha na Jackline Jerome
sauti ya meneja SIDO mkoa wa Morogoro – Joan Nangawe

Kwa upande wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), CPA Daudi Hashimu, Afisa Msimamizi wa Kodi kutoka Wilaya ya Kilombero, alitoa elimu kwa washiriki juu ya masuala ya kikodi kwa lengo la kuondoa migogoro kati ya walipakodi na mamlaka hiyo. Alisema elimu hii ni muhimu ili kujenga uelewa wa pamoja na kuboresha mahusiano ya kikodi.

sauti ya CPA Daudi Hashim – TRA Ifakara

Aidha, katika semina hiyo, afisa kutoka BRELA Yusufu Mwasakafyuka, mamlaka inayosimamia usajili wa biashara—alieleza kuwa changamoto kubwa wanayokutana nayo ni ukosefu wa elimu sahihi miongoni mwa wananchi kuhusu usajili wa biashara. Alionya dhidi ya tabia ya kutumia “vishoka”, akisisitiza kuwa kusajili biashara si jambo gumu kama watu wanavyodhani. 

sauti ya Yusufu Mwasakafyuka kutoka BRELA

Aidha, baada ya kupokea elimu kutoka kwa taasisi mbalimbali ikiwemo SIDO, TRA na BRELA, baadhi ya washiriki wa semina hiyo, akiwemo Fortuna Mwilenga, Ally Njoka, na Rehema Magwila, waliipongeza SIDO kwa kuandaa mafunzo hayo. Wamesema yamewasaidia kuelewa namna ya kuboresha biashara zao, kutunza akiba kupitia mfumo wa UTT, na kuepuka matumizi holela ya fedha. 

Sauti za baadhi ya washiriki semina