Pambazuko FM Radio

TRA Morogoro yatoa elimu kwa wafanyabiashara

16 September 2025, 8:53 am

wafanyabiashara katika halmashauri mji wa Ifakara Picha na Kuruthum Mkata

TRA Mkoa wa Morogoro imetoa elimu kwa wafanyabiashara wa Ifakara kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi na matumizi sahihi ya mashine za EFD, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari na kuongeza uelewa wa majukumu ya walipakodi.

Na; Kuruthum Mkata

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia ofisi yake ya Mkoa wa Morogoro imetoa elimu kwa wafanyabiashara wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara kuhusu mabadiliko ya baadhi ya sheria za kodi pamoja na matumizi sahihi ya mashine za EFD.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Bw. Chacha Gutora, Meneja Msaidizi wa Huduma kwa Walipakodi Mkoa wa Morogoro, amesema kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwawezesha wafanyabiashara kuelewa kwa kina mabadiliko ya sheria za kodi pamoja na matumizi sahihi ya mashine za EFD. 

Meneja msaidizi wa huduma kwa wateja Morogoro Chacha Gutora – Picha; Kuruthum Mkata

Aidha, amewahimiza wafanyabiashara kuhakikisha wanalipa kodi ya awamu ya tatu kwa wakati na kutoa risiti kila wanapouza bidhaa au huduma, huku akiwataka wateja kudai risiti kila wanapofanya manunuzi. Amesisitiza kuwa elimu hiyo ni endelevu na itatolewa kwa njia ya ufuatiliaji mtaa kwa mtaa.

Sauti ya Chacha Gutora

Kwa upande wake, Meneja wa TRA Wilaya ya Kilombero, Bw. Innocent Charles Minja, ameeleza kuwa lengo la semina hiyo ni kuhakikisha wafanyabiashara wanapata uelewa sahihi kuhusu ulipaji wa kodi, pamoja na kuwahamasisha kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari badala ya kulazimishwa.

Meneja TRA wilaya ya Kilombero Innocent Minja- Picha na Kuruthum Mkata

Sauti ya meneja TRA – Kilombero Innocent Minja

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mafunzo hayo, alitoa wito kwa TRA kuendelea kutoa elimu ya mara kwa mara kwa walipakodi kuhusu kodi na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.

Mkuu wa wilaya ya Kilombero wakili Dunstan Kyobya – Picha na Kuruthum Mkata

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Kilombero Dunstan Kyobya

Wakizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara, baadhi ya washiriki akiwemo Marius Benjamin Chikwekwe walipongeza TRA kwa kutoa elimu hiyo muhimu, huku wakielezea changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao ya ulipaji kodi.

Sauti ya Marius Chikwekwe mfanyabiashara