Pambazuko FM Radio

Vyama vya siasa vyapewa mafunzo maadili, makatazo

4 September 2025, 7:12 pm

Picha ya viongozi wa vyama vya siasa wakiwa kwenye mafunzo(picha na Kuruthumu Mkata)

Katika sheria ya gharama za uchaguzi kuna maadili na makatazo ambayo Chama,Mgombea au mtu yeyote anayeshiriki uchaguzi hapaswi kuyafanya kipindi cha uchaguzi

Na Katalina Liombechi

Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa nchini Tanzania imetoa mafunzo kwa viongozi wa vyama vya siasa wilayani Kilombero mkoani Morogoro kuhusu sheria ya gharama za uchaguzi pamoja na sheria ya vyama vya siasa.

Mafunzo hayo ambayo yamefanyika hii leo tarehe 4,Septemba 2025 Ukumbi wa Halmashauri ya Mlimba uliopo Ifakara yamelenga kuwakumbusha viongozi hao kuhusu maadili ya kisiasa na makatazo mbalimbali wakati huu wa uchaguzi, ili kuzuia uvunjaji wa sheria.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Afisa mwandamizi kutoka ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa Bi Edna Assey amesema ni wajibu wa viongozi wa vyama kufuata taratibu na kuendesha shughuli za kisiasa kwa mujibu wa sheria, ili kulinda amani na mshikamano wa kitaifa.

Picha ya Bi Edna Assey afisa mwandamizi kutoka ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa(Picha na Kuruthumu Mkata)

Amewakumbusha wajibu wa vyama vya siasa ikiwa ni pamoja na kuheshimu sheria za uchaguzi na kuzingatia kanuni za maadili za vyama vya siasa.

Sauti ya Bi Edna Assey 2

Hata hivyo ametaja vitendo vinayokatazwa kwa mujibu wa sheria ni pamoja na kutoa fedha kushawishi kupigiwa au kutompigia kura mtu na kutoa ahadi.

Baadhi ya viongozi wa vyama vilivyoshiriki mafunzo hayo wameahidi kufuata maelekezo waliyopewa na kuwataka wanachama wao kushiriki kampeni kwa amani, huku wakihimiza wananchi kuendelea kudumisha mshikamano bila kujali tofauti za kisiasa.

Picha ya viongozi wa vyama vya siasa(Picha na Kuruthumu Mkata)

Kwa upande wake Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Mlimba Zaituni Kisusi ameishukuru ofisi ya Msajili wa vyama kutoa elimu hiyo kwa viongozi hao wa vyama vya siasa huku akiwataka viongozi wa vyama kuwa mabalozi kwa wanachama wao.

Picha ya Zaituni Kisusi Msimamizi wa Uchaguzi Mlimba(Picha na Kuruthumu Mkata)
Msimamizi wa Uchaguzi Mlimba