Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
3 September 2025, 3:42 pm

Kongamano la elimu jumuishi ambalo limewakutanisha wadau mbalimbali kwa pamoja, wameahidi kuendeleza juhudi za kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto wote, bila ubaguzi.
Na Katalina Liombechi
Katika kuhakikisha elimu inawafikia watoto wote bila ubaguzi, kongamano la elimu jumuishi limefanyika leo katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara, kujadili changamoto na kuja na mikakati ya pamoja ili kurahisisha utoaji wa elimu kwa makundi mbalimbali.
Kongamano hilo ambalo limeandaliwa na shirika la Save Education kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu, limekuwa na lengo la kuhamasisha ushirikishwaji wa watoto wote katika mfumo wa elimu, hususani wale wenye uhitaji maalum.
Katika kongamano hilo miongoni mwa changamoto zilizowasilishwa ni pamoja na miundombinu ya ujifunzaji, uhaba wa walimu na uelewa mdogo wa baadhi ya wanajamii inavyowachukulia watu wenye ulemavu kama wanavyotueleza Rashid Namiuya Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Maria Faya Mjumbe mkutano mkuu TLB Mkoa wa Morogoro na mwanafunzi Diana Luanda kutoka shule ya msingi Kigamboni.
Afisa Elimu Msingi Halmashauri ya Mji wa Ifakara Witnes Kimoleta akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo amesema katika kukabiliana na changamoto hizo wamekuwa wakijitahidi kujenga mazingira wezeshi na kuchukua hatua za kupata fedha kwa ajili ya chakula kwa watoto wenye mahitaji maalum, kuwapeleka walimu 5 kupata mafunzo ya elimu maalum, kujenga bweni la watoto wenye mahitaji maalum ambalo lipo karibu kukamilika huku akieleza mchango wa wadau wanapotekeleza ujumuishi katika maeneo mbalimbali.

Mgeni rasmi katika kongamano hilo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, ambaye amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, jamii na mashirika binafsi katika kuhakikisha kila mtoto anapata haki yake ya msingi ya elimu.
Katika hotuba yake, Wakili Kyobya amewataka wazazi na walimu kuwapa watoto wote nafasi sawa ya kujifunza bila kujali hali zao na kupongeza juhudi zinazofanywa na Save Education katika kuunga mkono jitihada hizo.

Awali akizungumza Mkurugenzi wa Taasisi ya Save Education Clarence Mosha pamoja na Rosemary Mwenda kutoka HAKI ELIMU wamesema Kongamano hilo ni kupitia mradi wa sauti zetu wanaoutekeleza katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara na wamekuwa wakisaidia upatikanaji wa elimu jumuishi kwa kuibua changamoto zinazowakabili watoto hao kuziwasilisha kwa serikali kuzitafutia ufumbuzi wa pamoja ili watoto wapate elimu bila kikwazo.

Kongamano hilo limefanyika 03, Septemba 2025 ambapo limejumuisha walimu, wazazi, wanafunzi na wadau wa elimu kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Kilombero, ambao wamepata nafasi ya kujadiliana kwa kina changamoto na fursa katika utekelezaji wa elimu jumuishi nchini.