Pambazuko FM Radio

Teknolojia ya mkaa mbadala yazinduliwa Kilombero

14 August 2025, 7:02 pm

Picha ya washiriki mafunzo kuhusu teknolojia ya mkaa wa Pumba za Mpunga – Picha na; Isidory Mtunda

Katika semina iliyoandaliwa kupitia mradi wa UNIDO kwa ufadhili wa Serikali ya Japan na utekelezaji wa SIDO, wadau mbalimbali wa maendeleo wamekutana mjini Ifakara kujadili na kuelimishwa juu ya teknolojia ya kutengeneza mkaa mbadala kwa kutumia pumba za mpunga

Katika kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa na fursa za kiuchumi zinaongezeka kwa wananchi, shirika la UNIDO kwa kushirikiana na Serikali ya Japani, limezindua mradi wa kutengeneza mkaa mbadala kwa kutumia pumba za mpunga, mjini Ifakara, wilayani Kilombero.

Picha ya kuni zilizotokana na Pumba za Mpunga; Picha na Isidory Mtunda

Akizungumza wakati wa semina ya uzinduzi wa mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero wakili Danstan Kyobya amesema kilimo na shughuli za binadamu lazima ziendane na uhifadhi wa mazingira.

Mkuu wa wilaya ya Kilombero wakili Danstun Kyobya; Picha na Isidory Mtunda

Sauti ya mkuu wa wilaya ya KIlombero Wakili Danstun Kyobya

Kwa upande wake, Mhandisi Kalumuna Benedicto, Mkurugenzi wa Mradi huo kutoka SIDO, alieleza kuwa changamoto za mazingira kama uharibifu wa misitu na uchafuzi wa hewa ndizo zilizoibua wazo la kutumia pumba za mpunga kama nishati mbadala.

sauti ya Mkurugenzi wa SIDO – Mhandisi Kalumuna

Naye Mtafiti na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nelson Mandela Arusha, Dismas Kimaro, ameeleza kuwa mradi huu ni matokeo ya tafiti nyingi na kwamba Tanzania ni mzalishaji mkubwa wa mpunga, lakini kwa miaka mingi sehemu pekee inayotumika ni mchele tu.

Mhadhiri msaidizi wa chuo kikuu cha Nelson Mandela – D. Kimaro – Picha na Isidory Mtunda

Sauti ya Mhadhiri Dismas Kimaro

Florence Mbena, Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Mji wa Ifakara, amesema teknolojia hiyo inaleta fursa mpya kwa wananchi kwa kutumia pumba kama malighafi ya kutengeneza nishati mbadala, hatua itakayosaidia kuongeza kipato na kuimarisha uchumi wa kaya.

Sauti ya Afisa maendeleo mji wa Ifakara- Florence Mwambene

Mmoja wa washiriki wa semina hiyo, Edwin Lubomba, mjasiriamali, amesema kuwa teknolojia hiyo italeta fursa mpya za kiuchumi kwa wakulima na kwamba, mbali na kuuza mpunga na mchele, wananchi wataweza pia kuuza pumba kama malighafi ya kutengeneza nishati mbadala, jambo litakalosaidia kuongeza kipato, kulinda mazingira, na kuleta ajira kwa vijana.

Sauti ya Edwin Lubomba mshiriki

Mradi huu wa mwaka mmoja unatekelezwa katika mikoa mitatu nchini—Mbeya, Shinyanga, na Morogoro-kupitia Mji wa Ifakara na unafadhiliwa na Serikali ya Japani kwa gharama ya takriban shilingi bilioni 2.5.