Pambazuko FM Radio

TFS watumia mbinu shirikishi kutunza mazalia ya nyuki

20 May 2025, 6:47 pm

Na Katalina Liombechi

Picha ya Mzinga wa Nyuki katika eneo ilipo ofisi ya TFS Kilombero(Picha na Katalina Liombechi)

TFS Wilaya ya Kilombero wanaadhimisha Siku ya Nyuki wakisisitiza kuelimisha na kuhamasisha wananchi kufuga nyuki kwa wingi

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS Wilaya ya Kilombero imesema itaendelea kusimamia na kufanya ulinzi shirikishi kulinda Hifadhi za misitu na mazalia ya Nyuki ili jamii iendelee kunufaika kiuchumi.

Mhifadhi Misitu wakala hiyo Wilaya ya Kilombero Bi.Zarina Shaweji ameyasema hayo ikiwa ni maadhimisho ya siku ya nyuki Duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo Mei 20 maadhimisho ambayo kwa mwaka huu 2025 yanafanyika chini ya kauli mbiu isemayo ”Nyuki kwa uhai na uchumi imara”

Bi.Zarina ameelezea umuhimu wa kauli mbiu ya siku ya nyuki mwaka huu kwamba imebeba ujumbe wa dhamira ya Uchumi endelevu kutokana na faida za nyuki katika uchavushaji wa mazao ya kilimo,Mazao ya misitu na kuongeza kipato cha wananchi wanaofuga nyuki ambao hupata asali,nta,gundi sumu ya nyuki na Kadhalika huku wakala hiyo ikivijengea uwezo vikundi vya ufugaji wa nyuki zaidi ya 71 kwa kushirikiana na wadau.

Sauti ya Bi Zarina Shaweji Mhifadhi TFS Kilombero
Picha ya Bi Zarina Shaweji Mhifadhi TFS Kilombero(Picha na Katalina Liombechi)

Aidha amesema katika kuhakikisha Misitu inabaki salama wamekuwa na mikakati mbalimbali kama kufanya doria za mara kwa mara na kuvitembelea vikundi vya ufugaji nyuki kuvipatia elimu ili kuendelea kutunza manzuki za nyuki.

Sauti ya Bi Zarina Shaweji Mhifadhi TFS Kilombero

Ikumbukwe kuwa Maadhimisho ya siku ya Nyuki kwa mwaka huu 2025 hapa Tanzania yanafanyika Jijini Dodoma na Mgeni rasmi ni Waziri Mkuu Mh.Kasim Majaliwa.