Pambazuko FM Radio

Vinara wa uhifadhi kuja na mikakati ya kulinda Bonde la Kilombero

12 May 2025, 1:00 pm

Picha ya Vinara wa Uhifadhi Bonde la Kilombero wakiwa katika warsha Ifakara. Picha na Jackline Kyaruzi

Katika kuendelea kulinda ardhi oevu ya Bonde la Kilombero vinara wa uhifadhi wakusudia kujielekeza katika mbinu za kuhakikisha bonde hilo linabaki salama

Na Katalina Liombechi

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya amefungua rasmi Mtandao wa Vinara wa Uhifadhi wa Bonde la Kilombero (KNCC) kupitia warsha ya siku mbili iliyofanyika kuanzia Mei 8 hadi 9, 2025.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Wakili Kyobya ambaye pia ni mlezi wa mtandao huo, alisisitiza umuhimu wa ubunifu katika kutangaza mtandao huo pamoja na fursa zinazopatikana katika Bonde la Kilombero ikiwa ni pamoja kuwekeza katika maaeneo ya utalii huku akihimiza kuhamasisha kilimo cha mazao ya kimkakati kama kokoa, karafuu, chikichi, na parachichi, ili kuongeza tija ya kiuchumi kwa wananchi na kupunguza utegemezi wa moja kwa moja wa rasilimali zinazohifadhiwa.

Mh.Kyobya ameelezea kufurahishwa na jitihada zinazoendelea kufanywa na wadau mbalimbali za kurejesha mazingira ya asili akitolea Mfano Mto Ikwambi huku akisisitiza kuendeleza Kampeni ya “Soma na Mti Ishi na Mti” ili kurithisha utamaduni huo kwa vizazi vijavyo.

Niwaelekeze Vinara muwe na ushirikiano na mjielekeze kwenye kutoa elimu,kuhamasisha mazao ya kimkakati na usimamizi wa sheria.Amesema Mh.Kyobya.

Sauti ya Dunstan Kyobya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya amefungua rasmi Mtandao wa Vinara wa Uhifadhi wa Bonde la Kilombero (KNCC). picha na Jackline Kyaruzi

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtandao huo Bw Joseph Chuwa amesema kwa pamoja walieleza kuwa kuyapokea kwa dhati maelekezo ya Mkuu huyo wa Wilaya na wameahidi kuyatekeleza kikamilifu ili kufanikisha malengo ya uhifadhi endelevu wa bonde hilo muhimu.

Sauti ya Joseph Chuwa Mwenyekiti wa Vinara wa Uhifadhi Bonde la Kilombero

ikumbukwe kuwa Bonde la Kilombero ni mojawapo ya vyanzo muhimu vya maji vinavyolisha Mto Rufiji,ambapo Bwawa la Mwalimu Nyerere linategemewa kuzalisha jumla ya megawati 2,115 za Umeme,kilimo cha umwagiliaji na matumizi ya binadamu.