Pambazuko FM Radio

DC Kilombero afungua rasmi mtandao wa vinara wa uhifadhi Bonde la Kilombero

10 May 2025, 8:15 am

Na Katalina Liombechi

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya amefungua rasmi Mtandao wa Vinara wa Uhifadhi wa Bonde la Kilombero (KNCC) kupitia warsha ya siku mbili iliyofanyika kuanzia Mei 8 hadi 9, 2025.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Wakili Kyobya ambaye pia ni mlezi wa mtandao huo, alisisitiza umuhimu wa ubunifu katika kutangaza mtandao huo pamoja na fursa zinazopatikana katika Bonde la Kilombero ikiwa ni pamoja kuwekeza katika maaeneo ya utalii.

Aidha, alihimiza wanamtandao hao kuhamasisha kilimo cha mazao ya kimkakati kama vile kokoa, karafuu, chikichi, na parachichi, ili kuongeza tija ya kiuchumi kwa wananchi na kupunguza utegemezi wa moja kwa moja wa rasilimali zinazohifadhiwa katika bonde hilo.

Mh.Kyobya ameelezea kufurahishwa na jitihada zinazoendelea kufanywa na wadau mbalimbali za kurejesha mazingira ya asili akitolea Mfano Mto Ikwambi huku akisisitiza kuendeleza Kampeni ya “Soma na Mti Ishi na Mti” ili kurithisha utamaduni huo kwa vizazi vijavyo.

Mlezi huyo wa KNCC aliwasisitiza Vinara hao kujielekeza katika usimamizi wa Sheria kutoruhusu mifugo ndani ya hifadhi,ujenzi wa makazi hifadhini pamoja na uvuvi haramu  hali ambayo inahatarisha uendelevu wa ardhi oevu Bonde la Kilombero ikiwa ni eneo muhimu kwa ikolojia na maisha ya wakazi wake.

Picha ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero(Mlezi KNCC) Mh.Dunstan Kyobya(Picha kwa hisani ya Jackline Kyeruzi)
Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtandao huo Bw Joseph Chuwa amesema kwa pamoja walieleza kuwa kuyapokea kwa dhati maelekezo ya Mkuu huyo wa Wilaya na wameahidi kuyatekeleza kikamilifu ili kufanikisha malengo ya uhifadhi endelevu wa bonde hilo muhimu.

Sauti ya Mwenyekiti wa Mtandao wa Vinara Joseph Chuwa
Picha ya Vinara wa Uhifadhi(Picha kwa hisani ya Jackline Kyeruzi)

Ikumbukwe kuwa Bonde la Kilombero ni mojawapo ya vyanzo muhimu vya maji vinavyolisha Mto Rufiji, ambapo Bwawa la Mwalimu Nyerere linategemewa kuzalisha jumla ya megawati 2,115 za Umeme,pia bonde hilo ni muhimu kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na matumizi ya binadamu.