Pambazuko FM Radio

Miche 20,000 yapandwa Malinyi kuhimiza uhifadhi wa mazingira

22 March 2025, 5:24 pm

DC Waryuba akikagua miche na Majiko banifu katika shule ya Sekondari Njiwa _ Malinyi ; Na Isidory Mtunda

Na; Isidory Mtunda

Zaidi ya miche elfu ishirini imepandwa katika Shule ya Sekondari Njiwa, iliyopo Kata ya Njiwa, Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuhamasisha elimu ya utunzaji wa mazingira wilayani humo.

Wanafunzi wa shule ya Sekondari Njiwa – Malinyi – Morogoro wakipanda mche wa Mchungwa ; Na; Isidory Mtunda – Pambazuko fm Ifakara

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti katika Kongamano la Soka la Kijani 2025, Mratibu wa Mradi wa Uwezeshaji Jamii katika Usimamizi Endelevu wa Misitu na Nishati Mbadala, (USEMINI) Meshack Haule, amesema kampeni hiyo inalenga kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa misitu katika maisha ya kila siku.

Sauti ya Meshaki Haule mratibu wa mradi wa USEMINI wilaya ya Malinyi

Kwa upande wake, mgeni rasmi katika kongamano hilo, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Wakili Sebastian Waryuba, amesema mradi huo unalenga kuhamasisha usimamizi shirikishi na endelevu wa misitu pamoja na uzalishaji wa nishati mbadala katika wilaya za Malinyi, Morogoro Vijijini, Mvomero na Ulanga ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

DC Waryuba akipanda mche wa mti katika shule ya sekondari Njiwa _Malinyi – Morogoro . Na; Isidory Mtunda wa Pambazuko fm

Sauti ya DC Waryuba

Naye Meneja wa Mradi, Marko Mbilinyi, amesema moja ya majukumu ya mradi huo ni kuhakikisha wananchi wanamilikishwa ardhi kwa hati miliki ili kupunguza migogoro ya mipaka kati ya wakulima, wafugaji na pia taasisi za serikali ikiwemo TAWA ambayo mara kadhaa imejikuta katika migogoro na wananchi.

Picha ya bwana Mbilinyi akipanda mche wa mti – picha na Isidory Mtunda wa Pambazuko fm

Sauti ya Mbilinyi – meneja mradi

Aidha, Bwana Mbilinyi ameongeza kuwa wana mpango wa kufanya makongamano manne makubwa kwa mwaka huu, na kwamba kazi na shughuli zote zinafadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU).

Kwa upande wao, wanafunzi Yohana Singu na Catherine Maliganya wa Shule ya Sekondari Njiwa wamesema misitu ina faida nyingi kwa binadamu na mazingira huku wakionya kuwa ukataji hovyo wa misitu unasababisha mvua kuchelewa au kukosekana kabisa.

sauti ya Yohana na Catherine shule ya sekondari njiwa