Pambazuko FM Radio

Mikakati miaka 20 kuokoa, kutunza hifadhi ya Udzungwa

25 January 2025, 11:07 am

Na Katalina Liombechi/Kuruthumu Mkata

Picha ya wadau wa Mazingira katika Picha ya Pamoja Ukumbi wa Sunset hotel Mkoani Iringa(Picha na Kuruthumu Mkata)

Tanzania kuja na mikakati ya miaka 20 kuendelea kutunza na kurejesha mandhari ya Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa kufanya dunia kuwa sehemu salama kwa maisha ya binadamu na viumbe hai kwa ujumla.

Mikakati hiyo ni kupitia kikao kazi ambacho kimehusisha wataalam wa mazingira, watunga sera, wadau wa mazingira na baadhi ya wananchi kutoka katika mikoa mbalimbali iliyopitiwa na hifadhi hiyo mkutano ambao umefanyika mkoani Iringa katika ukumbi wa Sunset Hotel Januari 22 na 23, 2025.

Rose Gerald Mdendemi ni Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Wanyamapori Wizara ya Maliasili na Utalii akiwa katika kikao kazi hicho amesema kama Wizara wana mikakati mbalimbali ya kuhakikisha maeneo ya shoroba yanayounganisha hifadhi za Ruaha, Udzungwa na Nyerere yanaendelea kuhifadhiwa kwani maeneo hayo ni muhimu kiikolojia yakihifadhiwa vizuri itapunguza migongano kati ya binadamu na wanyamapori.

Aidha amesema kwa sasa Wizara inaandaa mwongozo wa kufuata katika kuongoa shoroba ambapo mara baada ya kukamilika utakabidhiwa kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji huku akitaja dhana ya ushirikiano katika kufanikisha azma hiyo.

Picha ya Rose Gerald Mdendemi Afisa wanyamapori Mkuu Wizara ya maliasili na utalii(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Rose Gerald Mdendemi Afisa wanyamapori Mkuu Wizara ya maliasili na utalii

Mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Mh. Joachim Nyingo kabla ya mabadiliko ya kiutawala akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Iringa amesema nia njema ya wadau wa mazingira inachagizwa na mazingira rafiki yaliyowekwa na serikali ya Tanzania kuunga mkono juhudi zake huku akieleza kuwa hifadhi ya milima ya Udzungwa inapoharibiwa athari zake inagharimu maisha ya watu wote duniani.

Sauti ya Joachim Nyingo Mkuu wa Wilaya ya Kilolo
Picha ya Mh.Joachim Nyingo Mkuu wa Wilaya ya Kilolo(Picha na Kuruthumu Mkata)

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika linalojihusisha na Uhifadhi wa Tembo Kusini mwa Tanzania STEP Frank Lihwa amesema lengo la Mkutano huo ni kuja na Mbinu za kutunza na kurejesha madhari ya safu ya Milima ya Udzungwa ikiwa ni eneo muhimu kwa bionuwai hivyo kushirikisha jamii na wadau mbalimbali,kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala,kutoa elimu na kuwapa watu njia mbadala ya kipato ni miongoni mwa njia zitakazosaidid kuleta matokeo chanya.

Picha ya Frank Lihwa Mkurugenzi STEP(Picha na Kuruthumu Mkata)
Sauti ya Frank Lihwa Mkurugenzi STEP

Mkutano huo Umeandaliwa na Shirika linalojihusisha na uhifadhi wa Tembo kusini mwa Tanzania STEP, Shirika linalojihusisha na Urejeshaji wa Misitu Afrika(REFOREST AFRICA)na (ASSOCIAZIONE MAZINGIRA).