Kila wiki mtoto mmoja anazaliwa kabla ya muda wa ujauzito kukamilika
9 April 2024, 2:09 pm
Na Elias Maganga
Matatizo ya maradhi ya kuambukiza na maradhi ya kudumu kwa muda mrefu kwa mama mjamzito inatajwa kuwa ndicho chanzo cha mtoto kuzaliwa kabla ya muda wa ujauzito kukamilika {Mtoto njiti}
Dkt. Samwel William Msomba kutoka kituo cha afya cha Kibaoni katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara mkoani Morogoro ambaye anahudumu katika kitengo cha watoto wachanga, ameyasema hayo wakati akizungumza na Pambazuko Fm juu ya mpango wa malezi na makuzi ya watoto wachanga wasiotimiza umri wakati wa kujifungua na uzito pungufu kwa kushirikana na Solidarmed.
Dkt. Msomba ametaja sababu nyingine ambayo inaweza kulazimisha kumtoa mtoto kabla ya muda wake pale inapotokea chupa ya uzazi kupasuka kabla ya muda wake .
Dkt. Msomba anasema pamoja na kutoa sababu za uzito pungufu na kuzaliwa kabla ya muda, mtoto wa aina hiyo kuna malezi maalum ambayo anatakiwa alelewe pale atakapokuwa kwenye maisha ya nje ya tumbo la uzazi kwa kutumia huduma ya Kangaroo Mother Care .
Watoto wenye uzito pungufu au waliozaliwa kabla ya muda wao Katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara ni kubwa kwani,wastani kwa kila wiki wanapata mtoto mmoja wa aina hiyo,ambapo pia Dkt. Msomba anataja mikakati waliyoiweka kuhakikisha tatizo hilo linapungua kwa kiasi kikubwa.