Jamii yatakiwa kupima magonjwa yasiyoambukiza
3 April 2024, 5:06 pm
Magonjwa yasiyoambukiza ni magonjwa yasiyo na vimelea vinavyoweza kusambazwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine, Baadhi ya magonjwa hayo ni pamoja na Magonjwa ya Moyo, mishipa ya damu, Magonjwa sugu ya njia ya hewa, Shinikizo la Juu la Damu, Kiharusi, Kisukari, na Magonjwa ya Akili
Na; Jackline Raphaely
Jamii imetakiwa kuona umuhimu wa kupima magonjwa yasiyoambukiza kama vile shinikizo la juu la. damu, moyo na mapafu sukari na saratani ya mlango wa kizazi ili kupunguza vifo vitokanavyo na magonjwa hayo.
Wito huo umetolewa na mratibu wa magonjwa yasiyoambukiza mkoa wa Morogoro Daktari Debora Kabudi mara baada ya huduma ya upimaji wa magonjwa hayo kukamilika katika Hospital ya Halmashauri ya Mlimba iliyotolewa na madaktari bingwa wa Moyo na Mapafu kutoka Hospital ya Rufaa ya Mt.Fransisko kwa kushirikiana na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo.
Naye mratibu wa magonjwa yasiyoambukiza Wilaya ya Bagamoyo Bi Rehema Kingu aliyeshiriki zoezi hilo amewasihi wananchi kutumia dawa ipasavyo ikiwa ana magonjwa hayo, kuzingatia mlo na kufanya mazoezi Pamoja na kupima afya kila baada ya miezi sita ili kuepuka magonjwa hayo.
Akitoa taarifa juu ya huduma ya upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza bure bwana Evance Mahundi ambaye ni daktari kutoka kliniki ya moyo na mapafu katika hospital ya rufaa ya Mt. Fransisko Ifakara amesema wamewafikia wananchi zaidi 162 na kuwapatia huduma stahiki.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mlimba Dkt. Wile Kopela ameshukuru ujio wa madaktari hao huku akisisitiza ushirikiano zaidi.
Wananchi nao hawakubaki nyuma kuelezea furaha yao baada ya kupata huduma ya vipimo na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza.
Klinik ya moyo na mapafu chini ya Hospital ya Rufaa ya Mt. Fransisko ngazi ya mkoa imejikita kutoa huduma za afya maeneo ya vijijini pia ina madaktari bingwa wa moyo na mapafu wahudumu wazuri wa afya vifaa tiba vya kisasa vinavyokidhi mahitaji ya wagonjwa