Pambazuko FM Radio

Moro yazindua ugawaji miche bora ya korosho

25 March 2026, 19:33

Picha ya DC Kyobya akipanda mti shule ya sekondari Ulanga kwa niaba ya RC wa Morogoro Adam Malima (Picha na Kuruthumu Mkata)


Lengo ni kuinua kipato cha wakulima kuchangia kukuza uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla
.

Na Katalina Liombechi

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mheshimiwa Adam Malima, amezindua rasmi zoezi la ugawaji wa miche bora ya mikorosho kwa wakulima wa mkoa wa Morogoro kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2025/2026.

Uzinduzi huo umefanyika tarehe 24 Machi 2026  katika viwanja vya Shule ya Sekondari Ulanga, iliyopo Wilaya ya Ulanga, ambapo viongozi mbalimbali wa serikali, wakulima pamoja na wadau wa sekta ya kilimo walihudhuria tukio hilo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya akimwakilisha Mkuu wa Mkoa Mhe. Malima amesisitiza umuhimu wa wakulima kutumia miche bora iliyozalishwa na bodi ya korosho kwa ushirikiano na Halmasuari ya Ulanga na kikundi cha upandaji miti cha wanawake Milola kuongeza uzalishaji wa zao la korosho, kutoka tani 938 inayozalishwa kwa sasa hadi kufikia tani 6,300 kimkoa lengo ni kuinua kipato cha wakulima kuchangia kukuza uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.

Picha ya Wakili Dunstan Dominic Kyobya (Picha na Kuruthumu Mkata)
Sauti ya DC Kyobya

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania amesema katika kufikia malengo ya serikali ya kuzalisha tani mil 1 ya korosho 2029/2030 Bodi ya Korosho Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo TARI Naliendele kwa kipindi cha 2025-2026 imepanga kuzalisha na kusambaza miche bora ya korosho Mil. 4.2 kwa kupitia vikundi vya wanawake na vijana.

Sauti ya Mkurugenzi Bodi ya Korosho

Wakitoa taarifa ya mradi kikundi cha wanawake waliozalisha miche bora ya korosho 44,421 wamesema wamefikia asilimia 98 ya lengo la miche 45,000.

Sauti ya mwana kikundi cha kupanda miti Milola

Mkulima bora wa zao hilo nchini Tanzania kutoka wilaya ya Ulanga ameelezea mafanikio anayoyapata kupitia zao hilo huku akiwa na malengo ya kutambulika zaidi katika nchi za Afrika.

Picha ya Mkulima bora wa korosho Tanzania (Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Njayaga Mkulima bora

Dkt. Rozalia Rwegasira kutoka Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro akiwa katika hafla hiyo amesema licha ya mkoa kuwa na mazao mengi yanayosaidia kiuchumi wameamua kuhamasisha zao hilo la korosho liwe miongoni mwa mazao ya kukuza uchumi kwa haraka ambalo pia ni rafiki kwa mazingira.

Picha ya Dkt.Rozalia Rwegasira (Picha na Kuruthumu Mkata)
Sauti ya Dkt. Rozalia Rwegasira

Mkuu wa Idara ya Kilimo,Mifugo na uvuvi Juma Kapilima ameeleza kuwa bodi ya korosho imekuwa chachu ya Halmashauri ya Wilaya ya ulanga kupiga hatua kupitia zao hilo na kwamba wilaya hiyo ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa zao la korosho ambapo kwa kipindi cha 2025-2026 wamezalisha miche nusu ya lengo la uzalishaji katika mkoa wa Morogoro.

Sauti ya Juma Kapilima Mkuu wa Idara ya Kilimo Ulanga

Uzinduzi huo uliambatana na upandaji wa miti hiyo bora katika shule ya Sekondari ya ulanga.