Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
21 March 2026, 11:43 am

Doria ya pamoja ya maafisa wa mazingira na kamati ya kijiji imebaini uharibifu wa msitu wa hifadhi wa Kilombero (KNFR), huku mamlaka zikitoa onyo kali dhidi ya vitendo vya ukataji miti na uchomaji mkaa.
Na Isidory Mtunda
Maafisa kutoka Kitengo cha Maliasili na Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, kwa kushirikiana na wajumbe wa Kamati ya Mazingira ya kijiji cha Mpofu pamoja na Jumuiya ya watumia maji bonde dogo la Ruipa, wamebaini vitendo vya uharibifu wa msitu wa hifadhi wa Kilombero (Kilombero Nature Forest Reserve (KNFR), ikiwemo ukataji miti na uchomaji wa mkaa.

Akizungumza na Pambazuko FM kwa njia ya simu baada ya doria hiyo, Katibu wa Kamati ya Mazingira ya Kijiji cha Mpofu, Richard Kidodowaja, amesema walikuta tanuri mbili za mkaa zikiwa tayari zimetumika pamoja na miti iliyokatwa kwa ajili ya maandalizi ya uchomaji mkaa.

Kwa upande wake, Afisa Mhifadhi wa KNFR, Tullah Abong’o, amesema ushirikiano kutoka kwa wananchi wa kijiji cha Mpofu umekuwa muhimu katika kufichua vitendo vya uhalifu ndani ya msitu huo, huku akibainisha kuwa taarifa wanazotoa zimekuwa chachu ya hatua za ulinzi.

Ameongeza kuwa baada ya doria hiyo, operesheni ya kumtafuta mtuhumiwa ilianzishwa, hata hivyo mtuhumiwa huyo anasadikiwa kutoroka nje ya Wilaya ya Kilombero baada ya kubaini kuwa anatafutwa.
Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Dunstan Kyobya, ametoa onyo kali kwa wanaojihusisha na uharibifu wa misitu, akisisitiza kuwa serikali haitavumilia vitendo vya uvamizi na uharibifu wa rasilimali za misitu.

Msitu wa Hifadhi ya Asili ya Kilombero ni miongoni mwa maeneo muhimu ya hifadhi yenye bioanuai kubwa nchini Tanzania, ukiwa na mchango mkubwa katika vyanzo vya maji na makazi ya viumbe hai. Hata hivyo, umekuwa ukikabiliwa na changamoto za uvamizi unaotokana na shughuli za kibinadamu kama vile uchomaji mkaa, ukataji miti na kilimo haramu, hali inayotishia uendelevu wa rasilimali hizo.