Pambazuko FM Radio

Wito watolewa na TFS Kilombero kulinda misitu

19 March 2026, 7:00 pm

Picha ya kitalu cha miche iliyooteshwa na TFS Kilombero(Picha na Katalina Liombechi)

TFS imekuwa ikichukua jitihada kadhaa kuendelea kutoa elimu,kuhamasisha upandaji wa miti kwa kugawa bure miche ya miti ya mbao na matunda kama mkakati wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi

Na Katalina Liombechi

Wakati Dunia ikitarajia kuadhimisha Siku ya Misitu Duniani, sekta ya misitu katika Wilaya ya Kilombero bado inakabiliwa na changamoto ya uharibifu wa rasilimali za misitu unaosababishwa na shughuli za kibinadamu, ikiwemo ukataji wa miti kwa ajili ya uzalishaji wa mkaa na mbao.

Hayo yameelezwa na Mhifadhi Daraja la Kwanza kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Kilombero, Shukrani Madinda wakati akizungumza na Pambazuko FM kuelekea maadhimisho ya siku hiyo, ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo Machi 21.

Amesema kuwa maadhimisho hayo yanatoa fursa muhimu ya kuikumbusha jamii kuhusu umuhimu wa misitu katika nyanja za kimazingira na kiuchumi.

Ameongeza kuwa TFS imekuwa ikiendelea kuhamasisha upandaji wa miti na kwamba wamekuwa wakizalisha miche laki 1 kila mwaka  ikiwemo ya matunda na mbao na kugawa bure  kwa wananchi hatua inayolenga kutoa chanzo mbadala cha kipato, kuboresha upatikanaji wa matunda, pamoja na kuimarisha mandhari ya mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Picha ya Mhifadhi daraja la kwanza Shukrani Madinda TFS Kilombero(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Mhifadhi Shukrani Madinda TFS 1 Kilombero

TFS inapoendelea kutekeleza majukumu yake wanasimamia misitu kwa kuzingatia sheria, kwa njia ya kufanya doria za mara kwa mara,kuwachukulia hatua wanaofanya uharibifu pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusu uhifadhi endelevu wa misitu hasa kwa kuwajumuisha wanawake na vijana.

Sauti ya Mhifadhi Shukrani Madinda TFS 2 Kilombero

Maadhimisho ya siku ya misitu hapa nchini Tanzania yanatarajiwa kufanyika Mkoani Lindi na yanaadhimishwa chini ya kauli mbiu isemayo “Misitu ni uchumi endelevu tuhifadhi kwa maendeleo ya taifa letu”