Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
14 March 2026, 9:12 am

Kwasasa tunaona mabadiliko ya huduma bora katika hospitali hii kwa wateja,vifaa,majengo na mahusiano
Na Kuruthumu Mkata
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya amepongeza juhudi zinazoendelea kufanyika katika kuleta mabadiliko chanya katika Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Fransisko Ifakara kurahisisha utoaji wa huduma za kiafya.
Akizungumza katika hafla ya futari iliyoandaliwa na Hospitali hiyo Mh.Kyobya amesema kwasasa kumekuwa na mabadiliko makubwa ndani ya hospitali hiyo yanahusiana na huduma kwa wateja, mahusiano mazuri kati ya wafanyakazi na wagonjwa, upatikanaji wa vifaa tiba pamoja na uboreshaji wa majengo ya hospitali.

Amesema huduma zinazotolewa kwasasa zinaakisi uhalisia na ukongwe wa Hospitali hiyo tangu ilipoanzishwa Miaka 99 iliyopita akieleza kuwa mabadiliko hayo yanatokana na usimamizi mzuri uliopo chini ya mkurugenzi wa Hospitali Solanus Fussy.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Hospitali hiyo Bwana Fussy amesema hafla hiyo ya futari imelenga kumshukuru Mwenyezi Mungu pamoja na watu wote waliochangia maendeleo ya hospitali hiyo hadi kufikia ilipo sasa na kwamba hospitali imeamua kutoa nafasi kwa wadau mbalimbali kutoa maoni yao ili yaweze kufanyiwa kazi kwa ajili ya kuendelea kuboresha huduma.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Rashid Semngoya, alimpongeza mkurugenzi wa hospitali hiyo na kusema kuwa Halmashauri ya Ifakara inajivunia uwepo wa hospitali hiyo kutokana na mchango wake mkubwa katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.