Pambazuko FM Radio

Jamii yakumbushwa misingi ya ufugaji nyuki

14 March 2026, 8:33 am

Shukrani Madinda Mhifadhi kutoka TFS Kilombero(Picha na Katalina Liombechi)

Wanaotaka kufuga nyuki ndani ya misitu inayosimamiwa na TFS wanapaswa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kulinda misitu na kuhakikisha shughuli hiyo inafanyika kwa usalama.

Na Katalina Liombechi

Ufugaji wa nyuki imetajwa kuwa miongoni mwa shughuli muhimu zinazochangia uhifadhi wa mazingira pamoja na kuongeza kipato kwa wananchi.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa ili shughuli hiyo iwe na mafanikio na isiharibu rasilimali za misitu, wafugaji wanapaswa kufuata taratibu na miongozo iliyowekwa na mamlaka husika.

Akizungumza katika kipindi cha Uhifadhi na Jamii kupitia Pambazuko FM Radio kuhusu masuala ya ufugaji wa nyuki, Mhifadhi Daraja la Kwanza kutoka Wakala wa huduma za misitu Tanzania TFS Wilaya ya Kilombero, Shukrani Madinda, amesema kuwa wafugaji wanaotaka kufuga nyuki ndani ya misitu inayosimamiwa na TFS wanapaswa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kulinda misitu na kuhakikisha shughuli hiyo inafanyika kwa usalama.

Mhifadhi Madinda ameeleza kuwa hatua ya kwanza kwa mfugaji ni kupata kibali kutoka TFS kabla ya kuanzisha mizinga katika maeneo ya misitu inayosimamiwa na taasisi hiyo.

Amesema kibali hicho husaidia mamlaka kujua maeneo yanayotumika kwa ufugaji wa nyuki na kuhakikisha shughuli hiyo haileti athari kwa mazingira ya msitu.

Picha ya Mhifadhi Shukrani Madinda kutoka TFS(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Mhifadhi TFS Kilombero

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuchagua eneo sahihi la kuweka mizinga, akieleza kuwa eneo linapaswa kuwa salama, lenye vyanzo vya chakula kwa nyuki kama vile miti na maua, pamoja na kuwa mbali kidogo na makazi ya watu ili kuepuka hatari zinazoweza kujitokeza.

Mbali na hilo, Madinda amesema wafugaji wanapaswa kutumia mizinga bora ya kisasa inayorahisisha uvunaji wa asali na kulinda ustawi wa nyuki pia amewashauri wafugaji kuhakikisha wanatunza mizinga yao vizuri kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha inabaki katika hali nzuri na inavutia nyuki kuishi humo.

Sauti ya 2 Mhifadhi kutoka TFS