Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
10 March 2026, 7:59 pm

”Ajenda ya dhana potofu ya meno ya plastiki,ukeketaji wa viungo kinywani ijadiliwe kwenye mikutano ,mashuleni na vikao mbalimbali”
Na Katalina Liombechi
Jamii Wilayani Kilombero imetakiwa kupinga vikali dhana potofu kuhusu uwepo wa meno ya plastiki pamoja na vitendo vya ukataji wa kimeo na udata kwa watoto wachanga, na badala yake kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.
Wito huo umetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya, leo March 10,2026 wakati akizindua mafunzo ya kupinga dhana potofu kuhusu meno ya plastiki, ukataji wa kimeo na udata kwa watoto wachanga katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara.
Mafunzo hayo yanakusudia kuwafikia viongozi wa kata na Mitaa/vijiji 817 katika Halmashauri ya mji wa Ifakara ili waweze kuelimisha jamii kupitia mikutano na majukwaa mbalimbali.
Mkuu wa Wilaya Kyobya ameishukuru Wizara ya Afya kwa elimu hiyo kwani jamii itapata uelewa wa kutosha kuhusu dhana potofu ya ukeketaji wa viungo kinywani huku akikemea vitendo hivyo kwa watoto huku akiagiza jambo hilo liwe ajenda ili jamii iwe na uelewa kabla hatari haijatokea.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Meneja Mradi wa kutokomeza ukeketaji wa viungo vya kinywani, Dkt. Nila Jackson, amesema jamii inapaswa kuachana na imani potofu kuhusu meno ya plastiki pamoja na vitendo vya ukeketaji wa viungo vya kinywani kama kimeo na udata kwa watoto, akieleza kuwa vitendo hivyo ni ukatili unaoweza kusababisha kutokwa na damu nyingi na wakati mwingine vifo kwa watoto wachanga.

Kwa upande wake Mratibu wa huduma za kinywa na meno katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Dkt.Malangalila, amekiri kuwepo kwa baadhi ya visa vya imani hizo potofu na kueleza kuwa baadhi ya waganga wa jadi hushiriki kufanya vitendo hivyo kinyume cha taratibu za afya .
Ameshauri jamii kuwapeleka watoto katika vituo rasmi vya afya wanapokabiliwa na changamoto za namna hiyo.

Naye Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto, Zuhura Mpako, amesema mradi huo utasaidia kuongeza uelewa kwa jamii na kuchangia kupunguza vifo vya watoto wachanga.
