Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
6 March 2026, 3:52 pm

Viongozi wa kijiji cha Mdindo wilayani Ulanga wanasema wakazi wote waliathiriwa na maandalizi ya mradi wa uchimbaji madini wamelipwa fidia, huku wananchi wakisisitiza umuhimu wa uelewa wa mikataba na msaada wa kisheria kwa jamii.
Na; Isidory Mtunda
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mdindo, Kata ya Msogezi, Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro, Juma Mustapha Nguku amesema hakuna mkazi yeyote wa kijiji hicho aliyekosa kulipwa fidia ili kupisha mradi wa uchimbaji madini unaotarajiwa kuanza katika vijiji vya Mdindo na Epanko.
Nguku ametoa kauli hiyo wakati wa kikao cha kupitia na kuboresha baadhi ya maeneo ya ripoti ya utafiti wa msingi ulioandaliwa na Shirika la Justice Empowerment Organization la Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki kutoka kijiji cha Mdindo, akiwemo Michael Deule na Rosina Kavuluga, wamesema wananchi wengi walitia saini mikataba ya fidia bila kuipitia kwa kina, na kutoa angalizo kwa wakazi wa kijiji cha Epanko kuwa makini ili kuepuka kurudia makosa hayo.
Kwa upande wao wakazi wa kijiji cha Epanko, Pankrasi Lucas Kanyali na Fridiana Matei Eranga wamesema bado kuna uelewa mdogo miongoni mwa wananchi kuhusu masuala ya fidia, na kuomba kupatiwa msaada wa kisheria kupitia wataalamu wa Paralegal ili waweze kufahamu haki na stahiki zao wakati mchakato wa fidia utakapoanza.
Meneja Mradi kutoka Shirika la Justice Empowerment Organization, Magdalena Akwilino Mlolele, amewashauri wakazi wa Epanko kushikamana katika kudai haki zao, kushirikiana na serikali ya kijiji katika kufuatilia masuala ya fidia, na iwapo watashindwa kupata ufumbuzi katika ngazi ya kijiji, wafikishe hoja zao kwa uongozi wa wilaya.

Kikao hicho kimewakutanisha Paralegal kutoka Mahenge, viongozi wa vijiji pamoja na baadhi ya wananchi kutoka vijiji vya Epanko na Mdindo wilayani Ulanga, kwa lengo la kuwasilisha na kujadili ripoti ya utafiti wa msingi uliofanyika Desemba 2025 kuhusu masuala ya fidia na haki za wananchi katika maeneo yanayotarajiwa kuathiriwa na mradi wa uchimbaji madini.