Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
2 March 2026, 1:52 pm

Kuna umuhimu wa kuongeza kasi ya usajili wa vikundi mbalimbali ili kuwezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika uchumi shindani na jumuishi
Na Katalina Liombechi
Katika kuhakikisha Dira ya taifa 2050 inatekelezwa kwa ufanisi, Mkoa wa Morogoro kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii umefanya kongamano lililowakutanisha Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka halmashauri zote tisa za mkoa huo, ambao wametajwa kuwa chachu muhimu ya kufikia dira hiyo.
Kongamano hilo lililobeba kaulimbiu isemayo, “Maafisa Maendeleo ya Jamii ni Chachu ya Kufikia Dira ya 2050,” lililenga kuchochea utekelezaji wa malengo ya kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani; kukuza uwezo wa watu na maendeleo ya jamii; pamoja na kuhimiza uhifadhi wa mazingira na kuimarisha ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza katika kongamano hilo, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Morogoro, Gibson Mwakoba, alisema lengo kuu la Dira ya 2050 ni kuhakikisha uchumi unakuwa jumuishi, kutokomeza umasikini, kuongeza kasi ya uwezeshaji wa vijana, kusisitiza usawa wa kijinsia, pamoja na kukuza ujumuishi wa kifedha kwa makundi yote ya jamii.

Katika kongamano hilo, Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kupitia Afisa Manunuzi wa PPRA Mkoa wa Morogoro, Christopher Masebo, ambaye akiwa mmoja wa wawezeshaji, alitoa elimu kuhusu ushiriki wa makundi maalum katika ununuzi wa umma.
Masebo amewakumbusha Maafisa Maendeleo ya Jamii kuhakikisha makundi maalum, ikiwemo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, yanajumuishwa kikamilifu katika fursa za ununuzi wa umma na kupewa kipaumbele stahiki kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Mercy Gibson Minja, amesema kuwa ili kufanikisha Dira ya 2050 ni lazima kila Afisa Maendeleo ya Jamii akatekeleza majukumu yake kwa weledi, uwajibikaji na ubunifu ili kuleta matokeo chanya kwa jamii.

Kongamano hilo ambalo limefanyika hivi karibuni, katika mji wa Ifakara kwenye ukumbi wa Mlimba limekuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu na mikakati ya pamoja ya kuharakisha maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.