Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
13 February 2026, 8:18 pm

Polisi Kupitia maadhimisho ya siku ya familia ya polisi,Jeshi hilo hujipima na kuhakikisha linatimiza wajibu wake wa kulinda raia na mali zao
Na Katalina Liombechi
Maadhimisho ya Siku ya Familia ya Polisi yamefanyika leo katika viwanja vya Kiungani, vilivyopo Halmashauri ya Mji wa Ifakara, wilayani Kilombero.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Kilombero, Daud Nkuba, amesema siku hiyo ni muhimu kwa Jeshi la Polisi kwani huwapa fursa ya kutafakari namna wanavyowahudumia wananchi na kuimarisha ushirikiano kati ya jeshi hilo na jamii.
Ameongeza kuwa kupitia maadhimisho hayo, Jeshi la Polisi hujipima na kuhakikisha linatimiza wajibu wake wa kulinda raia na mali zao, huku likiendelea kushirikiana na wananchi katika kudumisha amani na utulivu wakati wote.

Katika maadhimisho hayo, pia kupitia dawati la jinsia la jeshi hilo ilitolewa elimu kuhusu ukatili dhidi ya watoto, ambapo Jeshi la Polisi lilieleza kuwa linaendelea kujenga kizazi kinachochukia vitendo vya ukatili na uhalifu.

Mmoja wa wananchi walioshiriki maadhimisho hayo amepongeza juhudi za Jeshi la Polisi kwa kuwa karibu na jamii, akisema hali hiyo inawapa wananchi ujasiri wa kuripoti matukio ya uhalifu bila woga.
Maadhimisho ya Siku ya Familia ya Polisi hufanyika kila mwaka ifikapo Februari 13. Kwa mwaka huu 2026, maadhimisho hayo wilayani Kilombero yamefanyika katika viwanja vya Kiungani, yakianzia kwa maandamano kutoka eneo la NMB Ifakara, na kuadhimishwa chini ya kauli mbiu isemayo, “Polisi Jamii, Rejesha Amani na Utulivu.”