Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
13 February 2026, 3:06 pm

Ifakara Health Institute (IHI) imeadhimisha miaka 70 tangu kuanzishwa kwake, ikiendelea kujijenga kama taasisi kinara katika utafiti wa afya barani Afrika. Katika kipindi hicho, taasisi imeimarisha miundombinu ya maabara, kuongoza tafiti za malaria na chanjo, pamoja na kuzalisha wataalamu wa ngazi mbalimbali kuanzia Shahada ya Kwanza hadi Uzamivu.
Na: Isidory Mtunda
Ifakara Health Institute (IHI) imeendelea kuimarisha nafasi yake katika soko la kitaifa na kimataifa la utafiti wa afya, ikijipambanua kama taasisi kinara katika vita dhidi ya malaria kupitia ubunifu wa kisayansi katika kinga, tafiti za chanjo na mikakati madhubuti ya kudhibiti maambukizi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu Mtendaji, Dkt. Honorati Masanja, amesema kuwa kwa kipindi cha miaka 70, Ifakara Health Institute imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kukabili changamoto kuu za afya ya umma duniani, hususan katika mapambano dhidi ya malaria, afya ya mama na mtoto, pamoja na tafiti za maabara na majaribio ya kitabibu.

Aidha amesisitiza kuwa taasisi imekuwa injini ya kimataifa ya ubunifu, kuanzia majaribio ya vyandarua hadi tafiti za awali za chanjo ya malaria, huku ikiimarisha mifumo ya afya na kupunguza pengo kati ya takwimu za tafiti na uhalisia wa maisha ya jamii, hususan katika maeneo ya vijijini.
Nao wajumbe wa Bodi ya Wadhamini, Flora Myamba na Mariamu Bayumi, wameishauri Ifakara Health Institute kupanua wigo wa shughuli zake kutoka tafiti pekee na kuelekea katika uzalishaji wa bidhaa za afya. Wakitoa mfano wa tafiti za malaria, wamesisitiza umuhimu wa taasisi kuhamia katika hatua ya kutengeneza na kuzalisha bidhaa kama dawa na suluhisho bunifu zitokanazo na matokeo ya tafiti zake, ili kuongeza thamani ya matokeo ya kisayansi na kuchochea athari za moja kwa moja kwa jamii.

Kwa upande wake, mgeni rasmi aliyemwakilisha mkuu wa wilaya ya Kilombero, katibu Tawala wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, bw. Fabius Byamungu, ameipongeza Taasisi ya Afya Ifakara kwa mchango wake katika utafiti, mafunzo na huduma kwa jamii (research, training and service). Aidha amesema mafanikio ya taasisi hayawezi kufikiwa bila ushirikishwaji wa jamii, akibainisha kuwa kugusa maisha ya wananchi moja kwa moja ndiko kunakotoa uhalali na uendelevu wa malengo yake ya kimkakati.
Ifakara Health Institute (IHI) ilianzishwa mwaka 1957 mjini Ifakara kama Swiss Tropical Institute Field Laboratory (STIFL), kwa lengo la kufanya tafiti za magonjwa ya kitropiki hususan malaria. Katika kipindi cha miongo saba, taasisi imekua kutoka kituo cha maabara ya utafiti wa eneo moja hadi kuwa taasisi ya kimataifa ya afya ya umma inayotekeleza tafiti za kitabibu, kuimarisha mifumo ya afya, na kujenga rasilimali watu wa kiwango cha juu.
Kupitia kauli mbiu yake, “Kutoka Ifakara kwenda duniani,” taasisi inaonesha dira yake ya kuzalisha maarifa yanayoanzia katika jamii za Tanzania na Afrika, kisha kuyapanua kimataifa kupitia machapisho ya kisayansi, ushirikiano wa kimkakati na tafiti zenye athari za sera. Kauli mbiu hiyo inasisitiza mnyororo wa thamani wa utafiti—kutoka ngazi ya jamii (community-based evidence) hadi ushawishi wa sera na maamuzi ya afya duniani.