Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
12 February 2026, 9:01 pm

“Wakulima wengi wameamua kutoa zao la muwa na kuweka mpunga kutokana na kipindi cha nyuma walikuwa wakiuza gari moja anapata Tsh Mil.3 lakini kwa sasa gari hilo anapata hadi chini ya Laki 8”
Na Katalina Liombechi
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Mheshimiwa Kassim Nakapala, amesema halmashauri hiyo haioni manufaa kutokana na uwepo wa Kiwanda cha Sukari Kilombero kilichopo Wilaya ya Kilombero na sehemu ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.
Kauli hiyo imekuja kufuatia malalamiko ya mmoja wa wakulima wa miwa Bwana Msuya aliyedai kuwa kwa siku za nyuma walikuwa wakilipwa fedha nyingi kutokana na tani ya miwa wanayoipeleka kiwandani lakini kwa sasa kipato kinakuwa kidogo wanapouza miwa kwa kigezo cha kuangalia utamu unaopatikana kwenye muwa hali ambayo amesema imewalazimu wakulima wengine kuachana na kilimo hicho.
Akijibu malalamiko hayo katika kikao cha Baraza la Biashara, Bajeti na DCC Wilaya ya Kilombero kilichofanyika hivi karibuni, katika Ukumbi wa Mlimba uliopo Halmashauri ya Mji wa Ifakara Afisa Uhusiano wa Kampuni ya Kilombero Sugar, Victor Byemelwa, alisema kampuni huzingatia kiwango cha sukari (utamu) kwenye miwa, na si uzito wa tani pekee.

Hata hivyo, Mheshimiwa Nakapala alisisitiza kuwa bado halmashauri hainufaiki na zao hilo la kibiashara.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho, alisema atazifikisha changamoto hizo ngazi za juu kwa hatua zaidi.
