Pambazuko FM Radio

Wananchi Ijia walalamikia uvamizi wa mifugo

9 February 2026, 5:36 pm

Wakazi wa kijiji cha Ijia, kata ya Mchombe halmashauri  ya wilayani ya Mlimba, wamelalamikia uvamizi wa mashamba yao na mifugo ya wafugaji, wakidai hali hiyo imesababisha vurugu, majeruhi na kuongezeka kwa migogoro ya kijamii, huku wakimuomba mkuu wa Wilaya kuingilia kati na kutoa suluhisho la kudumu.

Na; Kuruthum Mkata

Wakazi wa kijiji cha Ijia, kata ya Mchombe, Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, wamelalamikia tabia ya wafugaji kulisha mifugo katika mashamba ya wakulima, wakidai hali hiyo imekuwa chanzo cha migogoro na kusababisha baadhi ya wakulima kushambuliwa.

Malalamiko hayo yametolewa katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo mbele ya mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya. Wananchi wamedai kuwa licha ya kutoa taarifa kwa uongozi wa kitongoji, hatua stahiki hazijachukuliwa.

sauti ya mwananchi 1

Mbali na migogoro hiyo, wananchi hao wameeleza kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mabomba ya maji, hali inayowalazimu kuchota maji katika Mto Mngeta wenye mamba, jambo linalohatarisha usalama wao.

sauti ya mwananchi 2

Katika hatua nyingine, Diwani wa Kata ya Mchombe Mh; Batholomeo Swala ametumia mkutano huo kuwasilisha kero nyingine zinazolikabili kijiji hicho, zikiwemo miundombinu mibovu ya barabara inayofanya baadhi ya maeneo kutofikika wakati wa masika, pamoja na ukosefu wa umeme katika vijiji vya Mbasa, Mpande na Shamba la Saba.

sauti ya diwani Batholomeo sawa

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, amekemea vitendo vya kuchukua sheria mkononi na kusisitiza kuwa hakuna aliye juu ya sheria. Ameagiza kila mfugaji kuwa na eneo lake maalum la shughuli za kilimo na kuelekeza uongozi wa kata, Polisi Kata pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri kusimamia utatuzi wa kero hizo.

Sauti ya mkuu wa wilaya – Dunstan Kyobya