Pambazuko FM Radio

UNIDO, Japan waipatia Moto max Mashine

7 February 2026, 5:20 pm

mtaalam kutoka kampuni Tromso akifanya majaribio ya kuchakata kuni mbadala baada ya kuzinduliwa

UNIDO na Japan waimarisha uzalishaji wa nishati mbadala Ifakara kupitia mashine ya briketi za pumba za mpunga.

Na; Isidory Mtunda

Kampuni ya Moto Max Energies inayozalisha mkaa mbadala katika kijiji cha Mahutanga, Halmashauri ya Mji wa Ifakara mkoani Morogoro, imekabidhiwa mashine ya kisasa ya kuzalisha kuni mbadala yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 130, kupitia mradi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) kwa kushirikiana na SIDO na kampuni ya TROMSO ya Japan.

Mashine hiyo imetolewa baada ya mchakato wa ushindani ulioshirikisha zaidi ya makampuni kumi yaliyoomba kunufaika na mradi huo, ambapo Moto Max Energies iliibuka mshindi kwa ngazi ya wilaya ya Kilombero.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Mratibu wa UNIDO, Faustine Msangila, amesema mradi huo unalenga kuhamasisha biashara za kijani na kuongeza thamani ya rasilimali zinazopatikana nchini, hususan pumba za mpunga zinazotumika kama malighafi ya kuzalisha briketi.

Sauti ya bwana Msangila

Kwa upande wake, mwakilishi wa Ubalozi wa Japan nchini Tanzania, Jin Hashimoto, amesema mradi huo umeandaliwa kupitia bajeti ya nyongeza ya Serikali ya Japan kwa lengo la kukabiliana na changamoto za kimazingira zinazotokana na matumizi ya nishati za asili, huku ukilenga kukuza uchumi endelevu kupitia teknolojia na ubunifu wa Kijapani.

Ameongeza kuwa matumizi ya pumba za mpunga kama malighafi yatapunguza taka, kuongeza thamani ya mazao ya ndani na kuimarisha usalama wa mazingira.

Bwana Jin Hashimoto akisoma hotuba picha na; Jackline Jerome
sauti ya Hashimoto na Lipipa ( mkalimani)

Kwa upande wa kitaasisi, mwakilishi wa Mkurugenzi wa SIDO, Mhandisi Benedict Kalumuna, amesema uwekezaji huo utafungua fursa za ajira, kukuza soko la mkaa mbadala na kuchochea uanzishaji wa viwanda vidogo vinavyozalisha vipuri katika eneo la Ifakara.

sauti ya Eng. Kaulumuna

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, ambaye alikuwa mgeni rasmi, amezitaka halmashauri za Ifakara na Mlimba kuhamasisha taasisi za umma na binafsi kutembelea kiwanda hicho kwa lengo la kujifunza na kuendeleza matumizi ya teknolojia ya nishati safi.

DC D. Kyobya akizindua mashine ya kuzalisha kuni mbada – picha Jackline Jerome
suati ya mkuu wa wilaya ya Kilombero – D. Kyobya

Kwa upande wao, wamiliki wa Moto Max Energies, Ibrahimu Kangamila na Joani Edward, wamesema mashine hiyo ina uwezo wa kuzalisha hadi tani moja ya kuni mbadala kwa siku, hatua itakayoongeza tija na upatikanaji wa nishati mbadala katika mji wa Ifakara.

Bi, Joane & Bw, Kangamila wakurugenzi wa Moto Max Energies – picha na Jackline Jerome

Wameongeza kuwa wanatarajia kutoa ajira kwa asilimia 70 kwa wasichana na wanawake, hususan vijana, ili kuongeza ushiriki wao katika shughuli za uzalishaji na biashara ya nishati safi.

Sauti za bw, Kangamila & bi, Joane