Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
6 February 2026, 8:02 pm

“Suala la lishe tumekubalina kwenye vikao na mikutano hivyo tunaendelea kukumbushana na kuhimizana”
Na Katalina Liombechi
Viongozi na Wananchi kata ya Lumemo katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara wameendelea kuhamasishana kuchangia lishe mashuleni ili kuwasaidia watoto kujifunza bila vikwazo.
Hayo yamesemwa na Diwani wa Kata hiyo, Mheshimiwa Frank Moses Ngao, wakati akizungumza na Pambazuko FM ofisini kwake.
Mheshimiwa Ngao amesema suala la lishe limekubalika kwa pamoja kati ya uongozi wa kata na wazazi kupitia vikao na mikutano mbalimbali, huku akisisitiza kuwa juhudi za kuhimiza ushiriki wa wazazi zinaendelea.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Kigamboni, Michael Mkemwa, amesema licha ya baadhi ya wazazi kujitokeza vizuri kuchangia lishe, bado wapo wachache wenye mwitikio mdogo hali inayowasababishia baadhi ya wanafunzi kushindwa kujifunza kwa umakini, kusinzia darasani na wakati mwingine kukumbwa na utoro.

Naye mmoja wa wazazi katika Kata ya Lumemo ametoa wito kwa wazazi wenzake kuona umuhimu wa kuchangia lishe, akisisitiza kuwa ni jukumu lao la msingi kwa ustawi wa watoto wao.
Wakati huo huo, baadhi ya wanafunzi wa Shule za Msingi Kigamboni na Lumemo wamesema hawajisikii vizuri kuona wenzao wakikosa chakula wanapokuwa shuleni, wakieleza kuwa hali hiyo huathiri ujifunzaji wao.
