Pambazuko FM Radio

RUWASA Moro wataka vyanzo vya maji vilindwe

6 February 2026, 11:07 am

Picha ya Viongozi wa RUWASA na jumuiya ya watumia maji Mlimba(Picha na Kuruthumu Mkata)

“Tunachotakiwa ni kulinda vyanzo vya maji ili vizazi vijavyo viweze kunufaika na huduma ya maji”

Na Kuruthumu Mkata

Meneja Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Morogoro, Mhandisi Sospeter Lutonja, amewataka wananchi kuhakikisha wanatunza na kulinda vyanzo vya maji, akisisitiza kuwa maji ni rasilimali muhimu yenye faida kubwa kwa taifa.

Mhandisi Lutonja ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya ufuatiliaji wa utoaji wa huduma za maji vijijini katika kata ya Mbingu, iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba ambapo amesema jamii ina wajibu wa kuhifadhi vyanzo vya maji ili vizazi vijavyo viendelee kunufaika na rasilimali hiyo muhimu.

Ameongeza kuwa RUWASA ni taasisi ya serikali iliyoanzishwa kwa lengo la kutoa huduma ya maji kwa wananchi, na si taasisi ya kibiashara hivyo jamii inapaswa kutambua jukumu hilo na kushirikiana na taasisi hiyo katika kutunza miundombinu ya maji.

Sauti ya Meneja wa RUWASA Morogoro

Madiwani wa kata za Mbingu na Igima wamepongeza utekelezaji wa mradi wa maji unaotekelezwa katika kata zao, wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3 licha ya uwepo wa changamoto ya upungufu wa maji katika baadhi ya maeneo.

Sauti ya Madiwani

Baadhi ya wananchi, akiwemo Bw. Shukrani, wameipongeza RUWASA kwa juhudi zake za kutatua changamoto za maji na kueleza kuwa kwa sasa maji yanapatikana kwa urahisi zaidi, lakini wameomba tatizo la kukatika mara kwa mara lifanyiwe kazi ili huduma iwe endelevu.

Sauti ya Mwananchi

Ziara ya RUWASA Morogoro inaendelea katika wilaya za Ulanga na Malinyi, kwa lengo la kuhakikisha huduma za utoaji maji vijijini zinaboreshwa.