Pambazuko FM Radio

Solidarmed wachangia kupunguza vifo vya watoto wachanga Ifakara

30 January 2026, 8:14 pm

Picha ya Mh.Adam Malima RC Morogoro ni wa pili kutoka kushoto(Picha na Katalina Liombechi)

Kabla ya Mradi kufanya maboresho Hospitali ilikuwa inarekodi wastani wa vifo vya watoto wachanga hadi 175 kwa mwaka hali iliyochangiwa na upungufu wa huduma maalum na miundombinu stahiki

Na Katalina Liombechi

Vifo vya watoto wachanga katika Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Fransisko iliyopo Ifakara Mkoani Morogoro kwasasa vimepungua kwa kiwango kikubwa, kutokana na maboresho ya huduma za kujifungua na uangalizi maalum kwa watoto wachanga, hususan wanaozaliwa na changamoto za kiafya.

Awali akizungumza leo Januari 30 2026 katika hafla ya kukabidhi jengo la kujifungulia lililofanyiwa maboresho, jengo la watoto wachanga wanaohitaji uangalizi maalum pamoja na vifaa tiba Kutoka Shirika la Solidarmed Mkurugenzi wa Hospitali hiyo Solinius Fussy amesema kabla ya Mradi kufanya maboresho Hospitali ilikuwa inarekodi wastani wa vifo vya watoto wachanga hadi 175 kwa mwaka hali iliyochangiwa na upungufu wa huduma maalum na miundombinu stahiki na kwamba msaada wa SolidarMed umeimarisha uwezo wa hospitali kutoa huduma za uangalizi wa karibu na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya vifo hivyo.

Sauti ya Solinius Fussy Mkurugenzi Hospitali ya St.Fransis

Kwa mujibu wa Meneja wa Mradi Malneste James kutoka shirika lisilo la kiserikali la kimataifa la SolidarMed akizungumza wakati wa hafla hiyo amesema mradi huo unaojulikana kwa jina la Mwanzo mwema “A good start” awamu ya 2 umegharimu zaidi ya shilingi milioni 100 za Kitanzania, ukiwa na lengo la kuimarisha huduma za mama na mtoto na kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika.

Amesema kupitia mradi huo wanatekeleza afua kadhaa ikiwemo utoaji wa vifaa tiba vya kisasa, ukarabati wa wodi za wazazi na watoto wachanga, pamoja na kuwajengea uwezo watoa huduma za afya kupitia mafunzo ya kitaalamu.

Aidha amesema mradi huo pia unahusisha utoaji wa elimu kwa jamii kupitia vipindi vya redio ili kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa huduma za uzazi salama na kufanya tafiti kuhusu huduma ya Kangaroo kwa watoto wenye uzito mdogo, ili kuboresha zaidi matokeo ya kitabibu.

Picha ya Meneja wa Mradi wa A good Start kutoka Solidarmed wa kwanza kulia(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Meneja wa Mradi wa A good Start kutoka Solidarmed

Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mheshimiwa Adam Malima baada ya kuzindua majengo hayo amelishukuru shirika la SolidarMed kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya afya.

Amesema maboresho hayo yanarahisisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi na kuahidi kuwa ofisi yake itaendelea kutoa ushirikiano kwa wadau wa maendeleo wanaosaidia kuimarisha huduma za kijamii katika Mkoa huu.

Picha ya RC Malima akizindua Mradi Jengo la mama(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya RC Malima

Mmoja wa wananchi waliohudhuria hafla hiyo wameelezea shukrani zao, wakisema wanashuhudia maboresho makubwa katika hospitali hiyo kupitia ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo, hatua inayorejesha matumaini kwa familia nyingi katika Mkoa wa Morogoro na maeneo jirani.

Sauti ya Aziza Said Mkazi wa Ifakara

Shirika la Solidarmed lenye makao yake makuu Nchini Uswisi tangu lilipoanza kazi Tanzania mwaka 1999 kwenye makao yake makuu Ifakara wanatekeleza miradi mitatu Mkoa wa Morogoro inayolenga kuboresha huduma za afya ya msingi,Mama na Mtoto pamoja na Vijana katika maeneo ya Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga,Ifakara na Manispaa ya Morogoro.