Pambazuko FM Radio

Mlimba wapatiwa mafunzo kwa vitendo kulima kokoa

29 January 2026, 7:23 pm

Picha ya Baadhi ya wakulima wakipatiwa Mafunzo ya kulima kokoa(Picha kwa hisani ya MACCO)

Ziara hiyo imelenga kuwezesha wakulima kujifunza moja kwa moja kutoka kwa wakulima bora waliopiga hatua, kwa kubadilishana uzoefu, kuuliza maswali na kuona kwa vitendo mbinu zinazotumika shambani.

Na Katalina Liombechi

Katika kuendeleza utekelezaji wa shughuli za mradi wa Sustain Eco kupitia mpango wa Ziara ya Kubadilishana Rika (Peer to Peer Exchange Visit) ambao unalenga kuongeza ujuzi na uzoefu wa wakulima katika kilimo bora cha kokoa Shirika la Mazingira Alliance for Community and Conservation MACCO limefanya ziara ya kujifunza, kuwapeleka washiriki 18 kwenye shamba la Wakulima wa Mfano katika eneo la Mbingu Katika Wilaya ya Mlimba.

Washiriki hao ni kutoka katika vijiji sita ambapo kila kijiji wametoka wakulima 3 kwenda kupata uzoefu kujifunza kwa vitendo mbinu bora za kilimo cha kokoa, usimamizi wa mashamba, pamoja na njia endelevu za kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao.

Akizungumza kuhusu shughuli hiyo, leo Januari 29,2026 Mratibu wa Mradi wa Shirika la Mazingira Alliance for Community and Conservation (MACCO)Felista Mwalongo amesema kuwa ziara hiyo ni muhimu katika kuwajengea wakulima uwezo wa kujifunza kwa vitendo na kuchochea mabadiliko chanya katika uzalishaji wa zao la kokoa.

Picha ya Bi Felista Mwalongo (Picha kwa hisani ya MACCO)
Sauti ya Felista Mwalongo Mratibu MACCO

Hili linafanyika chini ya Mradi wa Sustain Eco unaotekelezwa na AWF kwa kushirikiana na IUCN Ukifadhiliwa na Serikali ya SWEDEN ukijikita katika kuwawezesha wakulima kupitia mafunzo, ziara na kubadilishana maarifa ili kufikia kilimo endelevu na uhifadhi wa mazingira kwa maendeleo ya jamii.

Kupitia mradi huo, MACCO ilipatiwa jumla ya dola za Kimarekani 18,000 kwa awamu mbili, kila awamu ikiwa na dola 9,000, kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha kokoa katika Wilaya ya Mlimba kama mbinu mbadala ya utunzaji wa mazingira.