Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
28 January 2026, 1:59 pm

Jumla ya shilingi milioni 600 zimetolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum ndani ya Halmashauri ya Mji wa Ifakara kupitia mikopo ya asilimia kumi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali za kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mikopo hiyo iliyofanyika Januari 27, 2026 katika viwanja vya Stendi ya Mabasi Kibaoni, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Bi. Pili Kitwana, alisema jumla ya vikundi 41 vimenufaika, ambapo hundi ya mfano ya shilingi milioni sita ilikabidhiwa, huku kiasi cha shilingi milioni 404 kikitolewa kwa vikundi hivyo. Alibainisha kuwa kati ya vikundi vilivyonufaika, 20 ni vya wanawake, huku vingine vikiwa ni vya vijana na watu wenye ulemavu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Kassim Nakapala, ameishukuru serikali kwa kutimiza ahadi yake kwa wananchi kwa kutoa mikopo hiyo, akisema itasaidia kuwakwamua kiuchumi, kuongeza pato la kaya na kuchochea maendeleo ya jamii
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, amesema wilaya iko tayari kusimamia kikamilifu utoaji na urejeshaji wa mikopo hiyo ili kuhakikisha inaleta tija kwa walengwa. Aidha, ametoa wito kwa maafisa wasafirishaji kuzingatia na kutii sheria za barabarani.
Akizungumza kama mgeni rasmi, Naibu Katibu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wanawake, Bi. Felister Mdemu, amesema serikali inaendelea kutoa mikopo kwa wananchi kwa lengo la kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa taifa. Hata hivyo, amesisitiza mikopo hiyo itumike kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuleta matokeo chanya na endelevu, hususan kwa wanawake.

Baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo wameishukuru serikali kwa kuwawezesha kupata mtaji usio na riba, wakisema mikopo hiyo imewasaidia kupanua shughuli zao za kiuchumi. Pia wametoa wito kwa wananchi kuchukua mikopo kwa uangalifu na kuitumia kwa malengo ya kujikwamua kiuchumi.
