Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
20 January 2026, 5:55 pm
Wakazi wa kijiji cha Epanko wilayani Ulanga wamelalamikia kucheleweshwa kwa fidia ya ardhi yao kwa zaidi ya miaka kumi kupisha mradi wa uchimbaji madini, wakitaka haki zao za ardhi na mazingira zilindwe kabla ya kuondolewa.
Na: Isidory Mtunda

Wakazi wa kijiji cha Epanko, kata ya Nawenge wilayani Ulanga mkoani Morogoro, wameendelea kusota wakisubiri kulipwa fidia ya ardhi yao ili kupisha shughuli za uchimbaji wa madini ya graphite kupitia kampuni ya Duma TanzGraphite.

Akizungumza na Pambazuko FM wakati wa mafunzo ya kuwajengea uelewa wananchi kuhusu sheria za ardhi, yaliyofanyika katika Parokia ya Epanko, Wakili Scholastica Jullu kutoka shirika la Justice Empowerment la jijini Dar es Salaam, alisema wananchi hao wamekuwa wakifanyiwa tathmini za mara kwa mara kwa zaidi ya miaka kumi bila kukamilishiwa malipo ya fidia yao.
Wakili Jullu aliongeza kuwa katika mafunzo hayo wananchi walibainisha matakwa yao kwa mwekezaji kabla ya kuondolewa katika maeneo yao, yakihusisha kuwekwa kwa mpango madhubuti wa mustakabali wa huduma za jamii ikiwemo zahanati na shule zilizopo ndani ya eneo la mradi.
Kwa upande wao wananchi wa kijiji cha Epanko akiwemo Fridiana Elanga, Evarista Zimamoto na Fredrick Kazimoto, wametoa shukurani kwa wanasheria pamoja na afisa mazingira kwa kuwajengea uwezo, wakisema elimu waliyoipata itawasaidia kufuatilia na kusimamia haki zao za ardhi, mazingira na ulinzi wa kijamii kwa ujasiri zaidi.

Naye Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga, Simoni Lupakisyo, aliwakumbusha wananchi wajibu wao wa kulinda, kutunza na kuhifadhi mazingira, akisisitiza kuwa kila mradi wa maendeleo unapaswa kufanyiwa tathmini ya athari kwa mazingira kabla ya kuanza utekelezaji wake.

Kwa hatua nyingine, wakazi wa kijiji cha Mdindo, kata ya Msogezi wilayani Ulanga, nao wameeleza kupitia changamoto zinazofanana baada ya tathmini ya ardhi yao kufanyika kupisha mradi huo wa uchimbaji wa madini.
Wakazi hao wamesema walilipwa fedha za pango kwa makubaliano ya mkataba wa miaka mitatu, muda ambao ulimalizika mwaka jana 2025. Aidha, wamedai kuwa mwekezaji aliahidi kuongeza mkataba wa mwaka mmoja mmoja endapo asingejenga nyumba mbadala kabla ya mkataba wa awali kuisha.

Kwa sasa, wakazi hao wapo kwenye mkataba wa mwaka mmoja ulioanza mwezi Agosti 2025 na unatarajiwa kumalizika Agosti 2026, huku wakieleza wasiwasi wao kuhusu hatma ya makazi yao endapo ahadi hizo hazitatekelezwa kwa wakati.
Mafunzo ya kuwajengea uwezo wananchi kuhusu sheria za ardhi pamoja na haki za ulinzi na mazingira kwa wakazi wa maeneo yenye madini wilayani Ulanga, mkoani Morogoro, yamewanufaisha jumla ya wananchi 63 kutoka vijiji vya Epanko (30) na Mdindo (33).