Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
28 December 2025, 4:00 pm

Waumini wa Kanisa la Calvary Assemblies of God (C.A.G) Ifakara wameungana kusherehekea Noeli kwa kula pamoja, ikiwa ni sehemu ya utamaduni wa kuimarisha mshikamano wa kiroho na kijamii miongoni mwao.
Na: Isidory Mtunda
Kanisa la Calvary Assemblies of God (C.A.G) Ifakara limeendelea kuendeleza utamaduni wake wa kuandaa chakula cha pamoja katika sherehe kubwa za kanisa kama Noeli, mavuno, siku ya watoto na siku ya Jeshi la wanawake wapeleka injili – JEWAWI.

kizungumza na Pambazuko FM wakati wa sherehe ya Noeli, Katibu wa kanisa hilo, Mwalimu Danieli Njakachai, alisema kuwa lengo ni kuwaleta waumini pamoja, bila kujali hali zao za kiuchumi, ili kusherehekea kama familia moja ya kiroho.
Naye askofu wa makanisa ya Calvary Assemblie of God Wilaya ya Kilombero, Askofu Daktari Horogo John Ilan, alieleza kuwa utaratibu huo unazingatia hali halisi ya baadhi ya waumini wasiokuwa na uwezo wa kuandaa sherehe majumbani kwao, hivyo kuwajumuisha kunaleta faraja na usawa.

Kwa upande wake, muumini Evian Kamara alisema kuwa kula pamoja huongeza mshikamano, huimarisha mahusiano na kutoa fursa ya kushirikishana changamoto za maisha miongoni mwao.
Kanisa la C.A.G Ifakara limejijengea utamaduni wa kipekee wa kuwaalika waumini kushiriki chakula cha pamoja katika nyakati maalum kama vile Noeli, Siku kuu ya Mavuno, Siku kuu ya Watoto na sherehe ya jeshi la wanawake wapeleka injili (JEWAWI). Utamaduni huu umelenga kuendeleza mshikamano na upendo katika jamii ya waumini.