Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
5 December 2025, 12:01 pm

Baadhi ya wafugaji wa Mbwa katika halmashauri ya mji wa Ifakara wamehoji sababu za vifo vya baadhi ya Mbwa baada ya chanjo ya kichaa cha Mbwa, huku wengine wakisisitiza chanjo hiyo kuwa salama. Idara ya Mifugo imefafanua kuwa hakuna madhara yaliyoripotiwa rasmi katika maeneo yaliyotoa chanjo.
Na: Isidory Mtunda
Baadhi ya wafugaji wa Mbwa katika halmashauri ya mji wa Ifakara, mkoani Morogoro, wametoa wito kwa serikali kupitia Idara ya Mifugo kuchunguza kwa kina kwa nini baadhi ya Mbwa wanaripotiwa kufa muda mfupi baada ya chanjo ya kichaa cha Mbwa. Rai hiyo imetolewa na mfugaji Vicent Omary Lukumbo wa mtaa wa Milola, kata ya Kibaoni, ambaye amesema kuna haja ya serikali kuweka wazi kama vifo hivyo vinahusiana na chanjo au ni sehemu ya mpango wa kudhibiti Mbwa wanaozurura mitaani.
Hata hivyo, wafugaji wengine, Halila Hermani na Kadili Katomondo, wameliambia Pambazuko FM kuwa chanjo ya mwaka huu haikusababisha madhara yoyote kwa Mbwa wao. Wamesema huenda sababu za vifo zilizoripotiwa ni tofauti na chanjo, huku wakitoa wito kwa wenzao kuhakikisha wanatunza afya za Mbwa kama wanavyotunza afya za binadamu.
Kwa upande wake, Afisa Mifugo wa halmashauri ya mji wa Ifakara, Dkt. Dunia Mlanzi, amesema kuwa chanjo iliyotolewa ilikuwa salama na hakuna tukio lolote la Mbwa kufa lililoripotiwa katika maeneo yote yaliyotoa chanjo hiyo.
Halmashauri ya mji wa Ifakara hufanya kampeni ya chanjo ya kichaa cha Mbwa mara kwa mara ili kudhibiti maambukizi kutoka kwa Mbwa kwenda kwa binadamu. Kila mwaka, baadhi ya wafugaji huibua hoja na maswali kuhusu usalama wa chanjo, hasa pale ambapo vifo vya Mbwa hutokea karibu na kipindi cha utoaji chanjo. Serikali mara kwa mara imekuwa ikisisitiza ubora wa chanjo hizo na umuhimu wa kuzifuata ili kulinda afya ya jamii.