Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
4 December 2025, 9:50 pm

Uzinduzi wa tovuti ya KNCC unatarajiwa kuongeza ufanisi katika utoaji wa taarifa,uhamasishaji wa jamii, na ushirikiano baina ya wadau wa uhifadhi, huku ikirahisisha upatikanaji wa taarifa za miradi, tafiti, na shughuli mbalimbali za mtandao huo
Na Katalina Liombechi
Tovuti rasmi ya Mtandao wa Vinara wa Uhifadhi Bonde la Kilombero Kilombero Network of Conservasion Champions KNCC imezinduliwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, katika hafla maalum ambayo imefanyika katika ukumbi wa Edger Maranta, Ifakara.
Uzinduzi huu unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha juhudi za uhifadhi, matumizi endelevu ya rasilimali za Bonde la Kilombero, na kuimarisha upatikanaji wa taarifa kwa wadau mbalimbali.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya alisisitiza umuhimu wa usimamizi endelevu wa Bonde la Kilombero kwa kushirikisha jamii kikamilifu, hususan vijana.
Amebainisha kuwa ushiriki wa vijana katika shughuli za uhifadhi unaweza kuleta mageuzi makubwa kiuchumi kupitia mazao ya kimkakati kama kokoa, karafuu, chikichi, parachichi na mengineyo, pamoja na ufugaji wa nyuki.
Pia alitoa wito wa kuachana na shughuli zinazoathiri mazingira kama ukataji miti kwa ajili ya mkaa hali inayohatarisha misitu mbalimbali akitolea mfano Msitu wa Nakandumbu.
Aidha, Wakili Kyobya amesisitiza haja ya kuongeza juhudi za uhamasishaji katika kutangaza utalii na vivutio vilivyopo ndani ya maeneo ya hifadhi za Pori la Akiba la Kilombero,Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa,Hifadhi ya Nyerere,Hifadhi ya Jamii ya ILUMA.
Amesema kuwa utunzaji wa vyanzo vya maji ni jukumu la pamoja na linapaswa kupewa kipaumbele cha juu ili kuhakikisha kuwa vizazi vijavyo vinaendelea kunufaika na raslimali hizi muhimu ambazo ni sehemu ya utajiri wa taifa la Tanzania.

Meneja wa AWF Wilaya ya Kilombero Clarence Msafiri amesema wao wanaamini mbinu ya ushirikishwaji wa wadau kufanikisha uhifadhi wa mazingira ili tija ipatikane kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

AWF kazi yake kubwa ni kuhakikisha shughuli za uhifadhi ni lazima kushirikisha wadau,hivyo kwa ushirikiano huo unasaidia kupata masuluhisho ya asili na kuendeleza uhifadhi katika bonde la Kilombero tumewasaidia kutengeneza tovuti itakayosaidia kupata taarifa na kuweka kazi za uhifadhi lakini pia wafadhili wanaweza kuona shughuli zinazofanywa nao wakaunga mkono.Amesema Clarence Msafiri Meneja AWF Kilombero.
Utakumbuka haya yanafanyika ikiwa ni Sehemu ya Mradi wa SUSTAIN-ECO unaotekelezwa na AWF kwa kushirikiana na IUCN chini ya Ufadhili wa Serikali ya Sweden