Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
30 November 2025, 4:40 pm

“Tunapenda kuisisitiza jamii maambukizi bado yapo kwahiyo waendelee kuchukua tahadhari, tuondoe unyanyapaa na tuwajali wengine”
Na Amina Mrisho
Kadiri dunia inavyokaribia kuadhimisha Siku ya UKIMWI Duniani tarehe 1 Desemba, jamii imeshauriwa kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa kuwa bado vipo na vinaendelea kuathiri maisha ya watu.
Ushauri huo umetolewa na Mratibu wa Masuala ya UKIMWI ngazi ya jamii katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Bi. Esther Mtweve, alipokuwa akizungumza na Radio Pambazuko ofisini kwake.
Kwa upande wake, Mratibu wa Masuala ya UKIMWI ngazi ya Hospitali, Dkt. Rajabu Chomboko, amesema kuwa katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara kuna jumla ya watu 10,424 wanaoishi na Virusi vya UKIMWI, ambapo wanaume ni 3,090 na wanawake ni 7,334.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Ifakara (KONGA), Bi. Grace Mshana, amesema maadhimisho ya siku hiyo hutumika kukumbushana kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu mapambano dhidi ya UKIMWI.
Kauli mbiu ya siku ya Ukimwi Duniani kwa mwaka huu 2025 inasema: “Imarisha Mwitikio, Tokomeza UKIMWI.”