Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
25 October 2025, 1:45 pm

Mfugaji mmoja, Mahela Kahamba Mwanzalima (40), amefariki dunia baada ya kupigwa risasi na walinzi wa hifadhi ya wanyamapori ya Iluma, wilayani Ulanga, mkoani Morogoro. Tukio hilo limetokea wakati marehemu na wenzake walipokuwa wakijaribu kuchukua mifugo yao iliyokuwa imekamatwa kwa kuchungia ndani ya hifadhi.
Na; Isidory Mtunda
Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linawashikilia walinzi watatu wa hifadhi ya wanyamapori ya Iluma kwa tuhuma za mauaji ya mfugaji mmoja wilayani Ulanga mkoani Morogoro.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, marehemu Mahela Kahamba Mwanzalima mwenye umri wa miaka 40, alifariki dunia baada ya kupigwa risasi kwenye paja la mguu wa kulia, na kuvuja damu nyingi, hali iliyosababisha kifo chake.
Tukio hilo limetokea Oktoba 16, 2025 katika kijiji cha Minepa, baada ya marehemu na wenzake wawili kudaiwa kuwavamia kwa silaha za jadi walinzi wa hifadhi wakijaribu kuchukua mifugo yao iliyokuwa imekamatwa kwa kuingia hifadhini bila ruhusa.
Watuhumiwa waliokamatwa ni Samweli Bossa (27), Godson Matumbo (42) na Kasimu Mpoma (43), wote wakazi wa Ifakara na maeneo ya jirani.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbuyuni, Rafaeli Makindanga, amethibitisha kupokea taarifa za tukio hilo la mauaji baada ya kupigiwa simu na wananchi mnamo Alhamisi, Oktoba 16, 2025. Amesema alichukua hatua za haraka kwa kuwasiliana na Jeshi la Polisi, pamoja na kuratibu usafirishaji wa mwili wa marehemu kwa ajili ya uchunguzi katika Hospitali ya Rufaa Mtakatifu Fransisko mjini Ifakara.
Kwa upande wa familia, ndugu wa marehemu, Shigela Luponya, amesema ni kweli Mahela Kahamba alipigwa risasi na walinzi wa hifadhi ya Iluma wakati akijaribu kuwakomboa mifugo waliokuwa tayari wameshikiliwa na walinzi hao.
Mpiga Imambo, mmoja wa viongozi wa wafugaji kutoka kijiji hicho cha Mbuyuni na pia shuhuda wa tukio, amesema alishiriki katika kupeleka mwili wa marehemu hospitalini kwa uchunguzi. Amesisitiza kuwa Mahela alipigwa risasi na askari wa hifadhi alipokuwa akijaribu kuchukua mifugo yake iliyokuwa imeshikiliwa
sauti ya Imambo – Kiongozi wa wafugaji