Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
25 October 2025, 10:01 am

TANAPA yafunga tembo kola ya GPS katika Hifadhi ya Nyerere ili kudhibiti uharibifu wa mazao na kupunguza migogoro kati ya wanavijiji na wanyamapori.
Na; Isidory Mtunda
Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) imefanikiwa kumfunga kifaa maalumu cha kufuatilia mienendo (GPS collar) kwa tembo mmoja anayehusishwa na uharibifu wa mazao katika kijiji cha Katurukila, kata ya Mkula, wilayani Kilombero, mkoa wa Morogoro. Hatua hii inalenga kupunguza migogoro kati ya binadamu na wanyamapori katika maeneo yanayozunguka Hifadhi ya Taifa ya Nyerere.

Afisa Mhifadhi Daraja II na msimamizi wa Kanda ya Msolwa, George Baraka, amesema tembo huyo ni miongoni mwa makundi matatu ya tembo hatarishi ambao mara kwa mara huingia mashambani na kusababisha hasara kubwa kwa wakulima na kuhatarisha usalama wa wananchi.

Kwa upande wao, mwenyekiti wa kijiji cha Katurukila, Athuman Kayoga, na mtendaji wa kijiji, Bright Mwinyi, wamesema wanyama hao huingia hata saa 12 asubuhi, hali ambayo huwazuia wakulima kwenda mashambani na kuathiri mahudhurio ya wanafunzi kwa kuhofia kushambuliwa na Tembo.
Migogoro kati ya wananchi na tembo imeongezeka katika maeneo yanayozunguka Hifadhi ya Taifa ya Nyerere kutokana na upanuzi wa makazi na ongezeko la shinikizo la ardhi. Tembo huvamia mashamba kutafuta chakula, na kusababisha hasara kubwa. Teknolojia ya GPS collaring imeanza kutumika Tanzania kama njia ya kufuatilia mienendo ya tembo hatarishi ili kurahisisha hatua za mapema za kuzuia madhara.