Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
24 October 2025, 7:23 pm

“Tukahamasishe utulivu na pale kwenye viashiria vyovyote msisite kutoa taarifa,muwasisitize watu wakapige kura amani ndio msingi wa kila kitu“
Na Katalina Liombechi
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, leo ameongoza kikao maalum na viongozi wa dini pamoja na wajumbe wa Jumuiya ya Maridhiano ya wilaya hiyo, kwa lengo la kujadili na kuimarisha hali ya amani na umoja kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Katika kikao hicho, ambacho kimefanyika leo Oktoba 24, Ofisini kwake Wakili Kyobya aliwashukuru viongozi wa dini kwa mchango wao mkubwa katika kudumisha utulivu na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Kilombero.
Amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwaelimisha waumini na jamii kwa ujumla kuhusu maadili, uvumilivu wa kisiasa na umuhimu wa kudumisha amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Aidha amesema kwa upande wa Serikali Wamejipanga vyema kuhakikisha wananchi wanabaki salama na kwamba katika hilo hawatamuonea haya mtu yeyote mwenye nia mbaya ya kuhatarisha amani iliyopo.
Kwa upande wao, viongozi wa dini Askofu jimbo katoliki Ifakara,Sheikh wa Wilaya ya Kilombero na Katibu Jumuiya ya Maridhiano Christophora Ngongowele walimpongeza Mkuu wa Wilaya kwa jitihada zake za kuunganisha jamii na kuendeleza majadiliano yenye kujenga amani huku wakiahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha wilaya inabaki kuwa salama na yenye upendo.
