Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
22 October 2025, 5:27 pm

Wakulima wa kijiji cha Mhelule, kata ya Mwaya wilayani Kilombero wamelalamikia ukosefu wa msaada wa karibu kutoka kwa maafisa ugani, wakisema hawafiki mashambani kubaini changamoto zao. Maafisa wanasema idadi yao haitoshi kuwafikia wote, hivyo wakulima wanapaswa kuwafuata
Na: Isidory Mtunda
Baadhi ya wakulima wa kijiji cha Mhelule, kata ya Mwaya wilaya ya Kilombero, mkoa wa Morogoro, wamelalamika kutopata huduma ya karibu kutoka kwa maafisa ugani, wakisema hawatembelei mashamba yao ili kutambua changamoto wanazokutana nazo katika uzalishaji wa mazao.

Malalamiko hayo yalitolewa jana wakati wa kipindi cha maswali na majibu kwenye mafunzo maalum ya kilimo bora yaliyoendeshwa na kaimu afisa ugani wa kata ya Mwaya, Neema Mhongole.
Akijibu hoja hiyo, Mhongole alisema, kwa kawaida mkulima ndiye anatakiwa kumfuata mtaalamu. Maafisa ugani ni wachache, na hivyo si rahisi kuwatembelea wakulima wote mmoja mmoja, hasa kama hawajaonyesha uhitaji.
Wadau wa kilimo, Brown Kalambo na Jaliwa Jamson ambaye ni afisa masoko kutoka kampuni ya Meru Agrovet, walihimiza wakulima kufuata kanuni bora za kilimo na kuchukua tahadhari wanapotumia viuatilifu.

sauti za wadau wa kilimo; Kalambo & Jamson
Mafunzo hayo yalifanyika katika ofisi ya kijiji cha Mhelule kata ya Mwaya, Halmashauri ya mji wa Ifakara mkoani Morogoro na kuhudhuriwa na wakulima 166.