Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
16 October 2025, 8:18 pm

sekta ya kilimo, ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Watanzania wengi, Mgombea urais kupitia chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD), Bi. Mwajuma Notty Mirambo, ameahidi kuboresha mazingira ya kilimo kwa kukifanya kuwa cha biashara na chenye tija
Na Elias Maganga
Mgombea urais kupitia chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD), Bi. Mwajuma Notty Mirambo, akiambatana na mgombea mwenza wake kutoka Zanzibar, BI. Mashavu Alawi Haji, ameahidi kuwa endapo atapewa ridhaa na wananchi kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atahakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha Watanzania mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika eneo la Stendi ya Kwa Makali,october 16,2025 Ifakara Mjini, Bi. Mirambo alisema serikali ya UMD itasimamia kwa dhati matumizi sahihi ya rasilimali za nchi ili kuongeza tija kwa wananchi.
Akizungumzia sekta ya kilimo, ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Watanzania wengi, mgombea huyo aliahidi kuboresha mazingira ya kilimo kwa kukifanya kuwa cha biashara na chenye tija.

Kwa upande wake, mgombea mwenza Bi. Mashavu Alawi Haji, ametoa wito kwa wananchi wa Ifakara kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura tarehe 29 Oktoba, na kuwapa kura ya ndiyo wagombea wa UMD ili kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.
Naye Katibu Mkuu wa UMD Taifa, Bw. Moshi Kigundula, amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani wakati wote wa kipindi cha uchaguzi.
Amesema amani ya kweli hujengwa kwa kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake mgombea ubunge kupitia UMD Jimbo la Kilombero Bi Zaitun Juma Njohole ametaja vipaumbele ambavyo atavishughulka endapo akipewa ridhaa ya kuwa mbunge wa jimbo hilo kuwa ni pamoja na Kilimo,uvuvi na miundombinu ya barabara

Chama cha UMD kinaendelea na mikutano yake ya kampeni katika mikoa mbalimbali nchini, kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba.
Tarehe 17 Oktoba, kampeni hizo zitahamia katika eneo la Mang’ula Mwaya, ambapo chama hicho kitaendelea kuwasilisha sera na ahadi zake kwa wananchi.