Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
14 October 2025, 8:26 pm

Wasichana hao waliozalishwa katika umri mdogo na kutelekezwa walifikiwa na Shirika la EDO na kupatiwa mafunzo ya ujuzi wa ushonaji na kilimo cha bustani ya mbogamboga na matunda hivyo kuwasaidia kujitegemea wao na familia zao.
Na Nicolatha Mpaka
Wakina mama wadogo 29 wamehitimu mafunzo kutoka katika Shirika la Enlighten Development Organization (EDO) yatakayowawezesha kujitegemea kimaisha.
Katika mahafali ya kuhitimu mafunzo hayo hii leo Oktoba 14, 2025 mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Wakili Dastan Kyobya, amelipongeza shirika hilo kwa kulibeba jukumu la kuwainua na kuwawezesha wasichana hao waliozalishwa katika umri mdogo na kutelekezwa ambapo awali walijikatia tamaa.

Aidha mkuu huyo wa wilaya ameendesha harambee katika hafla hiyo kupatikana fedha kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za kuwawezesha wakina mama wadogo,na kutoa wito kwa wadau kuwasaidia kwenye mahitaji yao ikiwa ni pamoja na vyerehani 10, mashine za umwagiliaji 2, na mifuko 10 ya mbolea.
Baadhi ya wahitimu walieleza namna Shirika la EDO lilivyobadili maisha yao baada ya kupatiwa mafunzo ya ujuzi mbalimbali, ikiwemo ushonaji, kilimo na ujasiriamali na kusema kwa sasa wana uwezo wa kujipatia kipato na kuwa na dira mpya ya maisha huku wakiwatia moyo wasichana wengine wanaopitia changamoto kama waliyoipitia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la EDO, Bw. Benitho Miwandu amemwambia Mgeni rasmi kuwa ahirika hilo litaendelea kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha maisha ya vijana na kuwajenga katika mfumo wa kujitegemea huku akiendelea kuomba ushirikiano kwa serikali kuwapata wasichana wengine ili nao waweze kuwasaidia kwa namna hiyo.
Katika harambee iliyoongozwa na mgeni rasmi kwa ajili ya kuchangisha mahitaji ya shirika jumla ya shilingi milioni 5,800,000 zilikusanywa ili kusaidia kuendeleza utoaji wa mafunzo hayo kwa wasichana wengine .
Katika utekelezaji wa majukumu ya kuwaezesha wakina mama wadogo EDO wanashirikiana na AKIFRA kwa ufadhili wa Wizara ya uchumi ushirikiano na maendeleo ya ujerumani BMZ na worldness fund kutoka nchini Ireland.