Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
25 September 2025, 9:49 pm

Jamii bado inahitajika kuchukua jukumu la ulinzi na uangalizi wa mtoto ili aweze kutimiza ndoto zake bila vikwazo
Na Hija namsa/Katalina Liombechi
Watoto wa kike wanne kati ya 67 wameshindwa kuhitimu Elimu ya Sekondari Katika shule ya Matundu hill iliyopo Kata ya Idete Halmashauri ya Mlimba,Mimba na utoro vikitajwa miongoni mwa sababu.
Katika mahafali ya 17 ya shule hiyo ambayo yamefanyika hii leo tarehe 25 Septemba, 2025 Mwalimu mkuu Isacka Kunyonga akisoma risala ya wanafunzi mbele ya Mgeni rasmi wadau na wazazi amesema Jumla ya wanafunzi 99 kati yao wasichana 67 na wavulana 32 walitarajiwa kuhitimu masomo ya Sekondari kwa mwaka huu,lakini imekuwa tofauti ambapo idadi hiyo imepungua hadi kufikia 95 wasichana wakiwa 63 na wavulana 32 huku wengine wanne wa kike wakishindwa kuhitimu kutokana na mimba za utotoni,utoro na kuhama.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo Mhifadhi Zarina Sheweji Meneja kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Kilombero alielezea kuguswa na jambo hilo na kutoa wito kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuendelea kuwahimiza watoto wao hasa wa kike kupata elimu na kutoruhusu tabia hatarishi zinazopelekea kukatisha ndoto zao.

Katika hatua nyingine Mhifadhi zarina Katika hotuba yake, alionyesha kufurahishwa na juhudi kubwa ya kutunza mazingira ya shule hiyo hali iliyomfanya kuguswa na kuchangia maendeleo kwa kukabidhi kiasi cha Tsh.laki 2 na kuahidi kuunga mkono juhudi hizo kwa kuipatia shule miche 500 ya matunda kuendelea kuimarisha utunzaji wa mazingira pamoja na kuahidi kutoa mbao 50 kwa ajili ya kutengeneza meza na viti vya walimu hatua itakayosaidia kuwajengea walimu ari na mazingira bora ya kufundishia.