Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
18 September 2025, 11:05 pm

SIDO yamaliza mafunzo ya siku 3 kwa wajasiriamali 250 Kilombero na kutunuku vyeti; DC atoa agizo la kufunguliwa kwa ofisi ya SIDO wilayani humo kusogeza huduma karibu na wananchi.
Na; Isidory Mtunda
Washiriki 250 wa semina ya wajasiriamali, wawekezaji na wenye viwanda katika Wilaya ya Kilombero wamehitimu mafunzo ya siku tatu na kutunukiwa vyeti vya ushiriki kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO).
Akifunga mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, amelielekeza shirika hilo kufungua ofisi katika wilaya hiyo ili kusogeza huduma kwa wananchi wa Kilombero, Malinyi na Ulanga, na kuwapunguzia adha ya kusafiri hadi makao makuu ya SIDO mjini Morogoro.

Meneja wa SIDO Mkoa wa Morogoro, Bi. Joan Nangawe, amepongeza agizo hilo akisema litasaidia kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wajasiriamali, kwani kwa sasa wamekuwa wakihudumiwa kwa uchache kutokana na ukosefu wa ofisi ya kudumu katika eneo hilo.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Bi. Mercy Gibson Minja, amesema tayari wameanza utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Wilaya kuhusu kugawa vitambulisho 250 kwa wajasiriamali waliohitimu, ambapo ndani ya mwezi mmoja na nusu kila mmoja anatarajiwa kuwa amepokea kitambulisho chake.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki, Mariamu Mmbaga amesema elimu waliyoipata imewasaidia kujua umuhimu wa kurasimisha biashara na kuacha kufanya shughuli kienyeji. Pia amepongeza ushauri walioupata kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuhusu uhitaji wa nembo za ubora kwenye bidhaa zao.
