Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
17 September 2025, 10:50 pm

TRA Mkoa wa Morogoro imeendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara wa Kilombero kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi, matumizi ya mashine za EFD, na umuhimu wa usajili wa TIN, ikiwa ni sehemu ya kuongeza uelewa na kuimarisha ukusanyaji wa mapato.
Na; Kuruthum Mkata
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Morogoro imeendelea na kampeni ya kutoa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi, ikiwa na lengo la kuongeza pato la taifa, kuvutia uwekezaji, na kuondoa mkanganyiko wakati wa ukusanyaji wa kodi.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, bw. Chacha Gutora, Meneja msaidizi wa huduma kwa mateja mkoa wa Morogoro, ameeleza kuwa maboresho hayo yamegusa maeneo mbalimbali, yakiwemo:
Kodi katika huduma za kifedha, Kodi ya uingizaji wa fenicha kutoka nje, kwa lengo la kulinda wazalishaji wa ndani—hasa wakulima wa miti
Aidha amesema kuwa kodi ya bidhaa za ndani kama mvinyo, siagi, na karanga (kau kau) ambazo sasa zitatozwa asilimia 5, huku zile kutoka nje zikitakiwa kulipa asilimia 10
Vinywaji aina ya aiskrimu (ice cream) vinavyotengenezwa nchini vitatozwa asilimia 5, na vile vya nje asilimia 10

Bwana Gutora amesisitiza kuwa maboresho hayo yanalenga kuongeza mapato ya taifa, kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja, na kuharakisha maendeleo ya kijamii na kitaifa.
sauti ya Chacha Gutora
Kwa upande wake, Bw. Innocent Charles Minja, Meneja wa TRA Wilaya ya Kilombero, aliwataka wafanyabiashara kuhakikisha wanajisajili na kupata TIN namba ili kuepuka migogoro ya kikodi. Ameeleza kuwa TIN moja inaweza kutumika kwa biashara tofauti, mradi zimesajiliwa kihalali.

Aidha bwana Minja amekumbusha kuhusu ulipaji wa mapato ya awamu ya tatu, akisisitiza umuhimu wa kulipa mapema ili kuepuka adhabu ambazo zinaweza kufikia hadi shilingi laki moja. Amehimiza matumizi sahihi ya mashine za EFD, akisisitiza kuwa ni lazima kutoa risiti kwa kila mauzo, na wateja kudai risiti kwa kila manunuzi.
sauti ya Innocent Minja
Wakati wa mafunzo hayo, baadhi ya wafanyabiashara wameipongeza TRA kwa kutoa elimu hiyo, wakisema imewasaidia kupata uelewa wa masuala ya kikodi. Hata hivyo, wameeleza changamoto kadhaa, ikiwemo utozaji wa kodi ya pango la nyumba za biashara na makadirio ya kodi ambayo hayazingatii msimu au hali halisi ya biashara

Ikumbukwe kuwa TRA Mkoa wa Morogoro ilianza ziara hiyo ya elimu Septemba 15, 2025, na inatarajiwa kuhitimisha Septemba 17, 2025. Elimu hiyo imetolewa katika kata tatu za Mbasa, Mlimba, na Mwaya, zilizopo Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro.